Rio Ferdinand aondoka

*Bacary Sagna aaga Arsenal

Beki wa muda mrefu wa Manchester United, Rio Ferdinand anaondoka klabuni hapo baada ya kutoongezewa mkataba.

Ferdinand aliyekuwa pia timu ta taifa ya England kabla ya kujitoa, alitarajia kuongezwa mkataba na kocha wa muda, Ryan Giggs alipendekeza hivyo pia lakini wakuu wa Old Trafford wamekataa, bila shaka kutokana na kiwango chake kushuka na umri kusonga mbele.

Ferdinand (35) amekaa miaka 12 klabuni hapo na kucheza mechi 454 na kufunga mabao manane. Alisema kwamba mazingira hayakumruhusu kuwaaga washabiki na wadau kwa namna ambavyo angependa.

Anaondoka katika msimu ambao Man U wamefanya vibaya kwenye ligi kuu, kumaliza katika nafasi ya saba, kukosa kufuzu kwa michuano ya kimataifa na kushuhudia kocha David Moyes akifukuzwa kazi baada ya miezi kumi tu kibaruani.

BACARY SAGNA AAGA ARSENAL

Wakati hayo yakijiri Manchester, beki wa kutumainiwa wa Arsenal, Bacary Sagna ameaga kwamba anaondoka kutafuta maslahi zaidi.

Arsenal walizembea tangu mwanzo kuanzisha mazungumzo naye na yalipoanza walisuasua wakitaka kumpa mkataba wa mwaka mmoja wakati yeye anataka wa miaka mitatu.

Kadhalika alitaka kuongezewa fedha, jambo lililowatatiza Arsenal ambao wanajulikana kwa sera ya kupendelea wachezaji wenye umri mdogo.

Inaelezwa kwamba huenda akajiunga na Manchester City, Chelsea au Paris Saint-Germain na itakuwa mwendelezo wa nyota wa Arsenal kuiacha klabu hiyo.

20140513-101825.jpg

Comments