Liverpool wajipa moyo

Baada ya kuukosa ubingwa wa England kutokana na makosa yao ya kwenye mechi za kuelekea mwisho wa msimu, Liverpool wameapa kwamba watajipanga upya ili kuutwaa ubingwa huo karibuni.

Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard (33) alisema kwamba kabla hajastaafu anaamini watatwaa ubingwa huo uliochukuliwa na Manchester City Jumapili hii na kuwaacha pointi mbili nyuma yao.

Liverpool wamejengwa upya na kocha Brendan Rodgers aliyechukuliwa kutoka Swansea kuchukua nafasi ya mkongwe Kenny Dalglish kutokana na mwenendo mbaya wa timu misimu miwili iliyopita.

Liverpool waliwafunga Newcastle 2-1 na kusubiri kuona kama West Ham wangeweza kuwasaidia kwa kuwafunga City, lakini waliishia kufungwa 2-0 na ndoto zao za ubingwa kupotea.

Kocha Rodgers aliwapongeza Man City na kusema walistahili kutwaa ubingwa huo, lakini akasema anajivunia kikosi chake na yote kilichofanya msimu huu. Man City wametwaa kombe hilo mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu, mara zote wakilichukua kutoka kwa jirani na mahasimu wao, Manchester United waliomaliza ligi katika nafasi ya saba msimu huu.

‘Uzoefu tuliopata unatusogeza karibu zaidi na ubingwa wa England, iwe ni mwaka kesho au mwaka unaofuata nina uhakika tutalipata kombe mapema maana nami nimebakiza miaka michache tu hapa,” akasema Gerrard.

Man City wamemaliza ligi wakiwa na pointi 86, Liverpool 84, Chelsea 82 na Arsenal 79 na timu hizo zimeingia kwenye kinyang’anyiro cha Ligi ya Mabingwa Ulaya huku Everton wakiambulia pointi 72, Tottenham Hotspur pointi 69 na watacheza Ligi ya Europa na Manchester United wakitoka kappa msimu huu na pointi zao 64.

Southampton wamemaliza ligi wakiwa na pointi 56, Stoke 50, Newcastle 49, Crystal Palace 45, Swansea 42, West Ham 40, Sunderland 38 sawa na Aston Villa, Hull 37 na West Bromwich Albion 36. Norwich, Fulham na Cardiff wameshuka daraja kwa kujikusanyia pointi 33, wengine 32 na 30 kwa mtiririko huo.

Comments