Manchester City mabingwa

Hatimaye Manchester City wamefanikiwa kunyakua ubingwa wa England katika siku ya mwisho ya Ligi Kuu, ambapo walikuwa wakihitaji pointi moja tu kutawazwa wafalme.

Vijana hao wa Manuel Pellegrini hawakufanya makosa walipoingia uwanjani nyumbani dhidi ya West Ham, kwani Samin Nasri na nahodha Vincent Kompany walihakikisha wanaipatia timu yao mabao, huku ngome ikihakikisha haivuji.

Wakati City wakipata ushindi huo, Liverpool waliokuwa wakiunyemelea ubingwa pia kwa kusubiri kuteleza kwa City, walianza vibaya baada ya Martin Skirttel kujifunga bao walipocheza dhidi ya Newcastle United na kuwafisha moyo washabiki dimbani Anfield.

Hata hivyo, Liverpool walizinduka baadaye, wakasawazisha kisha kufunga bao la ushindi lakini kwa kuzingatia matokeo ya City, Liver walishindwa kutimiza ndoto ya kutwaa ubingwa huo ambao waliupoteza tangu 1990.

City walikuwa wakipewa nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa huo, hasa baada ya Liverpool kuteleza hivi karibuni kwa kukubali kichapo kutoka kwa Chelsea, kabla ya mechi iliyopita kwenda sare ya 3-3 na Crystal Palace katika mchezo ambao vijana wa Brendan Rodgers walikuwa wanaongoza kwa mabao matatu kwa bila.

Nafasi ya tatu imekwenda kwa Chelsea ambao walianza vibaya mechi yao ya mwisho dhidi ya Cardiff kwa kutangulia kufungwa, lakini walisawazisha na kuongeza bao la ushindi katika kulindwa heshima yao. Nafasi ya nne imeshikwa na Arsenal waliowalaza Norwich 2-0.

Timu hizo nne ndizo zimeingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) wakati Everton waliowafunga Hull mabao 2-0 na Tottenham Hotspur waliowakandika Aston Villa 3-0 wamefuzu kucheza Ligi ya Europa.

Manchester United wamemaliza msimu kwa sare ya 1-1 na Southampton.
Swansea waliwakung’uta Sunderland 3-1, West Bromwich Albion wakalala 2-1 kwa Stoke na Fulham wakatoka 2-2 na Crystal Palace.Norwich wameungana na Cardiff na Fulham kushuka daraja.

Comments