Suarez mwanasoka bora wa mwaka

Mpachika mabao mahiri wa Liverpool, Louis Suarez amechaguliwa kuwa mwanasoka bora wa mwaka nchini England baada ya kuibuka na ushindi wa asilimia 52 kwenye kura zilizopigwa na waandishi wa habari za soka.

Suarez (27) pia hadi sasa anaongoza kwa kufunga mabao 31 kwenye Ligi Kuu ya England na kwenye kinyang’anyiro cha uchezaji bora alikwaana na nahodha wake, Steven Gerrard na kiungo wa Manchester City, Yaya Toure.

Mwenyekiti wa chama hicho cha waandishi, Andy Dunn alisema Suarez amedhihirisha umahiri na ubora wa aina yake katika kazi anayoifanyia Liverpool kwenye EPL, na moja ya vigezo ni umaliziaji wake, kwani ushindi kwenye soka ni mabao.

Suarez atakabidhiwa tuzo yake Mei 15 mwaka huu na ushindi wake umetokana na kura za waandishi zaidi ya 300, wakichagua mshindi kutoka majina 10 yaliyowekwa mbele yao na chama hicho. Tuzo hiyo ilianza 1948.

Mwanasoka bora wa msimu uliopita alikuwa Gareth Bale wa Tottenham Hotspur, akitanguliwa na Robin van Persie, Scott Parker, Wayne Rooney, na Steven Gerrard misimu iliyopita.

Msimu uliopita ulikuwa mgumu kwa Suarez aliyetaka kuihama Liverpool na England kwa ujumla, akidai alikuwa akichukiwa na viongozi wa FA na vyombo vya habari. Kadhalika katika mechi za ukingoni alimng’ata mkono mchezaji wa Chelsea, Branislav Ivanovich na kufungiwa mechi 10, adhabu aliyoendelea nayo hadi msimu huu.

Tangu hapo amebadilika kitabia, akiimarika kwenye kiwango akishirikiana vyema na mshambuliaji mwenzake, Daniel Sturridge. Alipata kuadhibiwa pia kwa lugha ya kashfa na kibaguzi dhidi ya mchezaji mweusi wa Manchester United, Patrice Evra.

Comments