Liverpool wavurunda

Baada ya Chelsea kuchezea nafasi ya kuwakamata Manchester City, Liverpool wamebweteka na kukubali kusawazishwa mabao matatu waliyokuwa wakiongoza nayo dhidi ya Crystal Palace katika dakika 12 za mwisho.

Ulikuwa usiku mchungu kwa Liverpool, ambapo mshambuliaji Luis Suarez aliangua kilio na kusindikizwa nje na Nahodha Steven Gerrard na Kolo Toure baada ya kuona kwamba mbio za ubingwa zimekwama.

Liverpool walianza vyema mchezo wakawazidi nguvu Palace na kupata mabao dakika ya 18 kisha mapema katika robo ya kwanza ya kipindi cha pili halafu wakaonekana kuridhika na hali hiyo bila kujua nguvu ya timu zinazofundishwa na mkongwe Tony Pulis, hasa zikiwa nyumbani.

Pulis aliyepata kuwanoa Stoke, alifanya mabadiliko kadhaa huku akitoa mbinu kwa wachezaji wake, na mara walianza kufanikiwa kuwazidi nguvu Liverpool ambapo majanga yalianza kuwakuta dakika ya 79 hadi 88, ambapo Palace walipiga mabao yasiyo na ubishi na kufanya mechi imalizike kwa 3-3.

Kocha Brendan Rodgers alisema baada ya mechi kwamba ndoto zao za ubingwa zimemalizika licha ya kwamba wanaongoza ligi wakiwa na pointi 81 wakifuatiwa na man City wenye 80 na Chelsea 79. Man City wamebakiza mechi mbili wakati Liverpool na Chelsea waliotoka suluhu na Norwich juzi wamebakisha mechi moja moja.

Arsenal wamejihakikishia nafasi ya nne na ushiriki Klabu Bingwa Ulaya.

Comments