Ubingwa Ulaya waenda Hispania

Hakuna shaka kwamba Ligi ya Mabingwa Ulaya itapata mfalme kutoka Hispania, lakini ni kwa mara ya kwanza fainali inakutanisha timu za jiji moja.
Baada ya Chelsea kutolewa kwa aibu na Atletico Madrid huku Real Madrid wakiwatoa Bayern Munich, sasa kivumbi kitakuwa kati ya timu mbili hizo hasimu lakini jirani za jiji la Madrid.

Chelsea walidhani kwamba wangefanikiwa kusonga mbele, hasa mchezaji wao mwenye bahati na mechi kubwa, Fernando Torres alipowafungia bao la kuongoza, lakini mchezaji wanayemuwania kutoka Atletico, Diego Coasta akalifuta.

Alikuwa Costa tena aliyefunga penati dakika ya 60 baada ya bao lake la kwanza dakika moja kabla ya mapumziko, kasha Turan akakata mzizi wa fitna kwa kuwachimbia Chelsea kaburi kwa kufunga bao la tatu dakika ya 72.

Kocha Jose Mourinho hakutarajia kabisa kwamba Atletico wangewatoa, hasa baada ya kulazimisha suluhu jijini Madrid kwenye mechi ya kwanza. Alidai kwamba kipa wao anayedakia Atletico kwa mkopo ndiye kikwazo dhidi yao.

Hata hivyo baadhi yaw achezaji wa Chelsea, akiwamo Eden Hazard anayesema mbinu za Mreno huyo zinaanza kupitwa na wakati. Jambo la kuvutia ni jinsi pia Torres alivyocheza dhidi ya timu yake ya zamani na anatajwa kwamba atarudi huko msimu ujao.

Atletico wamepiga hatua kubwa, katika La Liga na pia Ligi ya Mabingwa, kwa sababu ni mara ya kwanza katika miaka 40 wanafika fainali. Hii ni mara ya 17 kwa timu mbili kutoka nchi moja zinafika fainali ya Ulaya.

Msimu uliopita pia zilikuwa Bayern na Borussia Dortmund zilizoingia fainali na Bayern kutwaa ubingwa.

Real Madrid walipata kufika fainali na kuwafunga Valencia 3-0 msimu wa 1999/2000.

Comments