Arsenal wawatega Everton

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kwamba wao watajitahidi kushinda mechi walizobakiza huku wakiomba Everton wajikwae.

Arsenal ambao waliwafunga West Ham 3-1 usiku wa Jumanne katika dimba la Emirates, wanachuana na Everton kupata nafasi ya nne na ya uwakilishi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Arsenal wapo mbele ya Everton kwa pointi moja lakini Everton wana mchezo mmoja mkononi. Everton waliwapa kisago Arsenal karibuni na kufufua matumaini yao ya kucheza Ulaya.

Everton ambao Jumatano hii usiku watacheza na Crystal Palace, wanakabiliwa na mechi nyingine dhidi ya Manchester City, Manchester United, Southampton na Hull.

Arsenal kwa upande wao wamebakiza mechi dhidi ya Hull, Newcastle, West Bromwich Albion na Norwich.
Mchezaji wa Ujerumani wa Arsenal, Lukas Podolski aliyesema kwamba ana hofu wataweza kuikosa nafasi hiyo ya kucheza UCL kwa mara ya kwanza katika misimu 17, ndiye alifunga mabao mawili na jingine likafungwa na Olivier Giroud.

Hata hivyo, Kocha wa Everton, Roberto Martinez alisema wao hawana shinikizo kwa sababu hawana cha kupoteza wala hawakujua kama wangepanda hadi nafasi hiyo muhimu, hivyo watacheza kama kawaida.
Wenger alisema kupata kwao ushindi dhidi ya West Ham baada ya kutinga fainali ya Kombe la Ligi kumewapa nguvu na kujiamini zaidi Arsenal na sasa picha iliyo mbele yao ipo wazi.

Sare kwa Everton itawarejesha nafasi ya nne, kwani wana uwiano wa mabao wa +22 tofauti na wa Arsenal wa +18. Arsenal wana pointi 67, Everton 66. Vinara Liverpool wanazo 77, Chelsea wanaowafuatia wana 75 na Manchester City wana 66 na michezo miwili mkononi.

Comments