Samba Boys ruksa ngono

*Scolari awaruhusu Brazil kuwa na wapenzi wao

Kocha wa Timu ya Taifa ya Brazil, Luiz Felipe Scolari amewaruhusu wachezaji wake kuendelea kufanya ngono wakati wa mechi za Kombe la Dunia linaloanza Juni mwaka huu nchini Brazil.

Scolari alisema kwamba hakuna marufuku yoyote ya wachezaji kuwa na wapenzi au wake zao wakati wa mashindano hayo na kwamba watatakiwa kuendelea na mfumo wao wa kawaida wa mapenzi na si vinginevyo.

Imekuwa kawaida baadhi ya timu kuweka marufuku ya wachezaji kuwa na wake au wapenzi wao nyakati za mashindano makubwa kwa ajili ya kutaka kuwaweka wachezaji kuwa katika mazingira ya kimchezo na kukita akili kwenye mechi inayofuata.

England ni moja ya timu inayolaumiwa kwamba imekuwa ikifanya vibaya kwenye michuano ya kimataifa kutokana na athari za kuwapo wake au wapenzi wao kwenye kambi ya timu na kubadili maana nzima ya timu ilichokwenda kufanya.
Samba Boys, hata hivyo, watakuwa huru kujirusha wakati wote wa mashindano lakini lazima wahakikishe wanakuwa fiti kimchezo wakati wote, ameonya kocha huyo maarufu aliyepata pia kuwafundisha Chelsea.

“Mapenzi kikawaida yanaruhusiwa kwa wachezaji wetu, kwa njia mbayo itawapa uwiano mzuri na kwa mfumo usio mbaya maana kuna wengine wanafanya mithili ya kuruka sarakasi, sasa hiyo haifai wala kuruhusiwa,” akasema Big Phil ambaye pia ni Mbrazili.

Katika michuano ya Kombe la Dunia 2002 Scolari alikuwa mkali sana kwenye masuala hayo, ambapo aliwapiga marufuku wachezaji wake kujiingiza kwa namna yoyote ile kwenye vitendo vya ngono wakati wote wa mashindano hayo, ili kuhakikisha wanatwaa kombe, na kweli wakalitwaa.

Ronaldo alikasirikia hatua ya kuzuiwa kufanya ngono, akasema pamoja na kufurahia kutwaa kulinyanyua kombe hilo kwa furaha, kitu kingine ambacho hatakisahau ni walivyozuiwa kufanya ngono na kocha huyo mkali hivyo kumfanya awe na wakati mgumu kipindi chote cha mashindano hayo.

Comments