Man United nje Ulaya

*Atletico wawavuruga Barcelona

Wakat ndoto za Manchester United za kufanikiwa Ulaya zimegonga mwamba, Barcelona nao wameloweshwa na wenzao Atletico Madrid kwa kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

United wameaga michuano hiyo baada ya kupokea kichapo cha 3-1 kutoka kwa Bayern Munich na kushindwa kusonga mbele baada ya kuwa walitoka 1-1 kwenye mechi ya kwanza.

Wakicheza ugenini Jumatano hii, United walianza vyema kw akupata bao la kuongoza kupitia kwa Patrice Evra ambaye majuzi aliahidi wangevuka, lakini wana Bavaria wakajibu baadaye.

Mabao ya Mario Mandzukic aliyesawazisha, Thomas Muller aliyechochea kwa bao la pili na Arjen Robben aliyewavuruga kwa lile la tatu yaliwezesha Bayern kupata ushindi wa jumla ya 4-2 na kuwatupa nje Mashetani Wekundu waliokuwa na matumaini makubwa ya kusonga mbele.

Man U tayari wapo nje ya michuano ya Kombe la Ligi, Kombe la FA na katika Ligi Kuu kuna kila dalili kwamba hawataweza kutetea kombe.

United walikuwa wakitafuta tena ile rekodi ya 1999 ambapo walifanikiwa kuwafunika Bayern waliokuwa mbele yao kwa bao moja kwenye mechi ya pili, wakasawazisha na kuwatupa nje.

Katika mechi nyingine, Atletico Madrid wamewatupa nje mabingwa wa Hispania, Barcelona baada ya kuwachapa bao 1-0.

Ulikuwa mshituko mkubwa nchini humo baada ya Koke kufunga bao katika dakika ya tano tu Barca kushindwa kujibu dakika zaidi ya 85 zilizofuata.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Atletico waliwaendesha mchakamchaka Barca kiasi cha mipora kugonga mwamba mara tatu katika dakika 20 za mwanzo na hadi mpira kumalizika Barca walilamba kadi tatu za njano na Atletico moja.

Matokeo hayo yanawingiza Atletico nusu fainali pamoja na wenzao Real Madrid na Bayern pamoja na Chelsea ambapo droo itapangwa Alhamisi hii.

Comments