Kocha pekee mweusi EPL afukuzwa

Kocha pekee mweusi katika Ligi Kuu ya England (EPL), Chris Hughton amefukuzwa kazi na klabu ya Norwich inayofanya vibaya kwenye michuano hiyo msimu huu.

Norwich wanashika nafasi ya 17 miongoni mwa timu 20 zinazoshiriki ligi hiyo, na kwa hali ilivyo wanaweza kushuka daraja kutokana na mechi ngumu zilizo mbele yao.

Hata hivyo, kumfukuza kocha kipindi hiki si rahisi kuwa suluhisho la matatizo yao. Wamebakiza mechi dhidi ya Fulham, kasha dhidi ya vigogo Liverpool, Manchester United, Chelsea na Arsenal.

Wana pointi 32 sawa na West Bromwich Albion walio juu yao wakifuatiwa na Fulham wenye pointi 27, Cardiff 26 na Sunderland 25. Hata hivyo, Sunderland wana mechi tatu mkononi ambazo wakishinda zote Norwich watakuwa wameingia kwenye majanga ya kushuka daraja.

Hughton ndiye kocha pekee mweusi kwenye ligi hii maarufu zaidi duniani, na amekuwa akisema kwamba milango haipo wazi sawa kwa watu wa asili tofauti kuweza kufundisha timu za juu nchini England.

Kocha wa Birmingham City, Michael Johnson anadai wenyeviti wa klabu za juu za soka hapa wanadhani wachezaji au watu ambao wangependa kuwa makocha na ambao ni weusi, hawajajiendeleza ipasavyo kielimu ili kuwa makocha wazuri, ndiyo maana hawawapi nafasi hizo.

Norwich wamemteua kocha wa vijana, Neil Adams kushika nafasi hiyo. Uamuzi huo umekuja baada ya kupigwa 1-0 na West Brom Jumamosi hii na sasa Adams atakuwa na kazi ngumu ya kuwavusha vijana wake kwenye mechi zinazokuja.
 

Comments