Evra: Tutawapiga Bayern kama Chelsea

Nahodha Msaidizi wa Manchester United, Patrice Evra amesema wataushangaza ulimwengu kwa kuwatoa Bayern Munich kwenye mechi ya pili ya robo fainali nchini Ujerumani, kama Chelsea walivyowashinda na kutwaa ubingwa wa Ulaya.

Evra (32) anasema inasikitisha sana hali ya United ilipofikishwa ambapo msimu huu wana kombe moja tu wanalowania, lakini akasema wamejipanga vilivyo ili kama Chelsea walivyoshinda 2012 katika Uwanja wa Allianz Arena, nao wafanye hivyo hivyo.

Manchester United wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, nafasi ambayo Chelsea walimaliza nayo miaka miwili iliyopita, lakini wakatwaa ubingwa wa Ulaya nchini Ujerumani baada ya Didier Drogba kukwamisha mkwaju wa mwisho wa penati.

United wanarudiana na Bayern ambapo katika mechi ya awali Old Trafford walitoka sare ya 1-1 katika mazingira ambayo hawakutarajiwa, kwa jinsi walivyokuwa wamecheza vibaya mechi za ligi. Katika mechi hiyo pia Bayern walitawala kwa kiasi kikubwa ambapo United walitumia muda mwingi kujihami.

“Msimu wote huu unanikumbusha juu ya Chelsea ambao hawakuwa wakicheza vyema kwenye ligi ya hapa lakini wakatwaa ubingwa wa Ulaya. Si kawaida kuamini kwamba unaweza kuponesha vidonda kwa mchezo mmoja, inasikitisha lakini tunatakiwa kuwafanya washabiki wetu watujivunie kwenye mechi ya pili huko Bayern.

“Kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa tunacheza vizuri, tunajiamini na inaelekea kwamba tunajitoa zaidi kuhakikisha tunafika mbali kuliko ambavyo tumefanya kwenye ligi au michuano mingine ya hapa nyumbani,” anasema Evra.

Manchester United wana rekodi nzuri zaidi kwa mechi za ugenini katika mashindano makubwa msimu huu lakini wamekuwa wakipata tabu wanapocheza nyumbani, ambapo hadi sasa wapo pointi saba nyuma ya timu inayoshika nafasi ya nne. Timu nne tu hufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya hapa.

Comments