Yanga wawasha moto

Leo ilikuwa kama unamsukuma mlevi, ambapo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania , Yanga, waliwakandamiza JKT Ruvu kwa mabao 5-1.

Wakicheza tena na kipa wao namba moja, Deogratius Munish baada ya Juma Kaseja kucheza mechi ambazo Dida alikuwa ameumia.

Walikuwa na wakati mzuri tangu mechi kuanza, ambapo kama kuna siku Mrisho Ngasa alicheza vyema ni Jumapili hii, ambapo alifunga hat-trick pia Munishi alikuwa mzuri mno langoni.

Mabao mengine yalifungwa na Didier Kavumbagu na Hussein Javu katika mechi ambayo Yanga walicheza kwa kujidai na kujimegea nafasi nyingi za kuatisha vijana wa kocha wao msaidizi wa zamani, Freddy Felix Kataraiya Majeshi Minziro aliyefarijiwa na bao la Nashon Naftali dakika saba kabla ya mpira kumalizika.

Yanga sasa watajiuliza kwa mechi zijazo, kwa sababu wamefikisha pointi 49 wakati Azam wanazo 53 wakiwa wamecheza mechi sawa. Mbeya City wana pointi 46 wakishika nafasi ya tatu.

Yanga wanatakiwa kuwaombea Azam matatizo kwenye mechi zilizobaki, nao washinde, au pia wafanikiwe kwenye rufaa yao dhidi ya Mgambo JKT.

Comments