Ferguson huyoo Harvard

Kocha aliyestaafu Manchester United, Sir Alex Ferguson amejiunga na Chuo Kikuu cha Harvard ambako alikoingia mkataba wa kufundisha kwa muda mrefu.

Ferguson (72) ataanza kazi yake hiyo mpya mapema mwezi ujao katika programu mpya chuoni hapo inayohusu Biashara, Burudani, Vyombo vya Habari na Michezo katika moja ya vyuo vinavyoheshimika zaidi duniani.

Fergie ndiye kocha aliyepata mafanikio makubwa zaidi nchini Uingereza na alifikia makubaliano ya kazi hiyo nchini Marekani, na anatarajiwa kurejea huko mwezi ujao kwa ajili ya kutoa mhadhara kwa maofisa watendaji waandamizi kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Mskochi huyo ameona ni bora kuchukua kazi hiyo badala ya kuendelea kuketi kwenye jukwaa la watu maarufu au viongozi kutazama timu yake aliyomwachia David Moyes inavyofanya kazi. Alikaa Old Trafford kwa miaka 26 yenye mafanikio makubwa.

“Nimefurahishwa sana kupata fursa kama hii ya kuchangia nilicho nacho katika chuo chenye sifa kubwa miongoni mwa wasomi duniani. Muda niliokaa hapa tayari umenichochea uzoefu wangu na natumaini kuendeleza uhusiano mzuri katika shughuli za wanafunzi, vitivo na marafiki katika chuo hiki,” akasema Fergie akiwa Marekani.

Ferguson aliwawezesha Man U kutwaa jumla ya vikombe 38, kati ya hivyo 13 vikiwa ni vya ubingwa wa ligi kuu, viwili vya Ligi ya Mabingwa Ulaya na pia kuna vingine vya mashindano tofauti ndani na nje ya nchi. Kwa sasa ni balozi na mmoja wa wakurugenzi wa klabu hiyo.

Profesa wa Harvard, Anita Elberse amesema wamefurahishwa na Fergie kukubali kuchukua jukumu hilo jipya na kwamba wanasubiri kwa hamu ili aianze rasmi kazi yake hiyo, ambapo watapata uzoefu wake kwenye uongozi.

Comments