Bayern watwaa ubingwa Ujerumani

Bayern Munich wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani kwa mara ya 24, ambapo msimu huu wametwaa taji wakiwa na mechi saba mkononi.

Bayern wanaofundishwa na Pep Guardiola walijihakikishia kombe hilo baada ya kuwafunga Hertha Berlin mabao 3-1 na kufikisha pointi 77 ambazo wapinzani wao hawawezi kuzifikisha. Wanafuatiwa katika nafasi ya pili na Borussia Dortmund wenye pointi 52.

Mabao ya Bayern yalifungwa na Toni Kroos, Mario Gotze na Franck Ribery wakati wapinzani wao walifuta machozi kwa bao la penati iliyopigwa na Adrian Ramos. Guardiola amekuwa na wakati mzuri tangu ajiunge na Bayern, na utwaaji wa taji mapema kiasi hiki utaongeza jambo kubwa kwenye wasifu wake.

Guardiola (43) ameshafanikiwa kuongoza klabu ya Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga nchini Hispania mara tatu, taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) mara mbili kabla ya kwenda mapumziko ya mwaka mmoja kasha akaibukia Bavaria na kutwaa kombe mapema katika msimu wake wa kwanza.

Bayern hawa wanajiandaa kwa mechi kubwa ya UCL dhidi ya Manchester United wiki ijayo, ikiwa ni hatua ya robo fainali. United wapo katika hali mbaya kiuwezo wa uchezaji, lakini Bayern wanachukua kila aina ya hadhari wakijua kwamba wanao wachezaji wenye vipaji.

Kuna uwezekano wa Guardiola kuweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutwaa vikombe vitano kwa msimu mmoja, kwa sababu tayari amewezesha Bayern kutwaa Uefa Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu la Fifa Club World Cup, sasa Bundesliga na baadaye atajielekeza kwenye UCL.

Bayern hadi sasa wamecheza mechi 52 bila kupoteza hata moja, ambapo msimu huu wameshinda mechi 10 za ligi mfululizo wakiwa ugenini. Msimu uliopita waliweka rekodi ya kushinda mechi tisa mfululizo.

Comments