David Moyes: Hatoki mtu hapa

Kocha David Moyes amedai ana uhakika na kibarua chake Manchester United wakati pakiwa na taarifa tofauti kwamba kuna mipango ya kumfukuza kazi.

Moyes aliyezungumza kabla ya mechi dhidi ya Olympiakos Jumatano hii, alidai kwamba ana uhakika na hatima yake hapo, kwa maelezo kwamba Man U ni timu kubwa inayofanya kazi zake kwa visheni ya muda mrefu.

Wakati Moyes akidai hivyo, kuna fununu kwamba vigogo wa Old Trafford wanajipanga kuangalia timu itafanyaje kwenye mechi mbili au tatu kabla ya kutoa uamuzi, na kwamba wazo la kumfuta kazi sasa limeingia kwenye bodi na kwa wamiliki kwa mara ya kwanza.

Moyes anatakiwa kuhakikisha vijana wake wanapata ushindi wa walau mabao 3-0 ili kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwani katika mechi ya kwanza walifunga 2-0.

“Mimi ndiye kocha wa Manchester United bado, hatima yangu wala haijabadilika hata kidogo kwa sababu ni kazi kubwa hapa na mkataba wa miaka sita. Klabu hii haifanyi kazi zake kwa mfumo wa visheni ya muda mfupi mfupi,” akasema Moyes ambaye hata hivyo hakuwa mwenye raha.

Man U inapita katika kipindi kigumu, ambapo imepoteza heshima ya dimba lake la nyumbani lililokuwa linajulikana kama ngome, ambapo haikuwa kawaida kupoteza mechi hapo, lakini msimu huu wameshuhudia wakichapwa na timu ndogo sawa na timu kubwa, kichapo cha karibuni kabisa kikiwa wikiendi iliyopita ambapo Liverpool waliwakanyaga kwa mabao 3-0 hivyo kubaki pointi 18 nyuma ya Chelsea wanaoongoza ligi.

Wanashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi na kuna wasiwasi kwamba watakosa hata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, labda watwae taji lenyewe, jambo ambalo litakuwa ni muujiza kwa mwenendo wao.

Moyes amedai kwamba huzungumza mara kwa mara na mtangulizi wake, Sir Alex Ferguson pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Klabu, Ed Woodward, aliodai wanamuunga mkono kwa asilimia 100 na Fergie hujitokeza kila wakati kumsaidia.

Baada ya mechi dhidi ya Olympiakos, Mashetani Wekundu wana safari ngumu ya West Ham kabla ya kukumbana na vinara wa upachikaji mabao, Manchester City katika mechi ya watani wa jadi.

Comments