Ronaldo mwanasoka tajiri zaidi

*Afuatiwa na Messi, Eto’o, Rooney

Mchezaji Bora wa Dunia, Cristiano Ronaldo amezidi kupaa kwa umaarufu baada ya kutajwa kuwa mwanasoka tajiri zaidi duniani.

Ronaldo anayekipiga Real Madrid na ambaye ni majuzi tu alinyakua Tuzo ya Mwanasoka Bora (Ballon d’Or kwa 2013) safari hii amewapikua akina Lionel Messi wa Barcelona na Samuel Eto’o wa Chelsea.

Ronaldo (29) anadaiwa kuwa na utajiri wa pauni milioni 122 akifuatiwa kwa karibu na Messi mwenye pauni milioni 120.5 na Eto’o akifuatia nafasi ya tatu, huku akiwa pia namba moja kwa klabu za Ligi Kuu ya England.

Inaarifiwa kwamba Eto’o alikubali kupunguzwa mshahara alipohamia Chelsa kutoka Anzhi Makhachkala ya Urusi Agosti mwaka jana, hivyo mshahara wake ukapungua kutoka pauni 350,000 hadi £100,000 kwa wiki, alipoenda kuungana na kocha wake wa zamani, Jose Mourinho.

Raia huyo wa Cameroon ana utajiri wa pauni milioni 70 na alipokuwa Urusi alikuwa analipwa fedha nyingi kuliko mwanasoka yeyote duniani.

David Beckham alishika namba moja mwaka jana kwa kuwa na pauni milioni 175 lakini sasa ameshastaafu soka. Katika orodha ya wanasoka 10 tajiri zaidi, EPL inao wawili tu, Eto’o na Wayne Rooney wa Manchester United aliyejikusanyia pauni milioni 69.

Kwa mkataba wake mpya, Rooney atapata pauni milioni 85 katika miaka mitano ijayo, ikiwa ni sawa na mshahara wa £300,000 kwa wiki. Mpachika mabao wa zamani wa Arsenal, Thiery Henry anashika nafasi ya 10 kwa kuwa na pauni milioni 47, hivi sasa akiwa anakipiga New York Red Bulls nchini Marekani anakoongoza kwa kipato tangu ajiunge 2010.

Comments