Carles Puyol: Nang’atuka Barca

 

Nahodha wa Barcelona, Carles Puyol ameamua kung’atuka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu wa La Liga.

Puyol (35) ametaja sababu za kutundika daluga hapo kuwa ni kutoweza kucheza tena katika kiwango cha ushindani baada ya kufanyiwa operesheni mbili, ambapo pia amekosa michezo mingi.

“Baada ya operesheni mbili zilizopita, imekuwa vigumu zaidi kwangu kurejea katika hali ya kawaida na kuweza kucheza katika kiwango cha juu cha soka la ushindani kinachotakiwa, jambo ambalo sikuwa nimelitarajia, hivyo nimefikia uamuzi huu. Bado miezi mitatu wala sitakata tamaa, nitaendelea kucheza,” akasema Puyol.

Anaondoka licha ya mkataba wake kuwa uliongezwa hadi 2016, ambapo tayari amefikia makubaliano na uongozi wa klabu kumaliza mkataba huo mapema zaidi, lakini pia umri wake kisoka ni mkubwa.

Puyol amecheza mechi 593 kwa mabingwa hao wa Hispania tangu alipojiunga nao 1999, ambapo amefanikiwa kutwaa mataji sita ya ubingwa wa La Liga, matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mawili ya Kombe la Mfalme (Copa del Rey).

Kadhalika aliisaidia Barca kutwaa kombe la Uefa Super Cup mara mbili na Spanish Super Cup mara sita.

Kadhalika amewika sana katika timu ya taifa ya Hispania ambako amefanikiwa kutwaa nao Kombe la Dunia 2010 na Ubingwa wa Ulaya 2008 na ameichezea timu hiyo mara 100.

Kinachomponza hadi kuachia ngazi mapema ni matatizo ya goti katika miaka ya karibuni, ambapo alikosa mashindano makubwa ya Euro 2012 na katika msimu huu wa La Liga amecheza mechi 12 tu kwa Barca.

Hata hivyo, hajasema kama ndio utakuwa mwisho wa kucheza soka, lakini amesema kwamba baada ya Juni 30 atakutana na waandishi wa habari kuaga baada ya kukaa Barcelona kwa miaka 19 ila hajajua atafanya kazi gani baada ya hapo, bali anataka kupumzika kwanza.
 

Comments