Arsenal wazama, Chelsea, Liverpool juu

Arsenal wamezamishwa na Stoke City katika Dimba la Britannia kwa kutandikwa bao 1-0 kwa penati ya Jonathan Walters katika mechi ngumu.

Stoke walifunga baada ya beki wa kati Laurent Konscielny kuunawa mpira na sasa timu hiyo imeweka rekodi ya kuwafunga Manchester United na Chelsea pia na kujiweka pazuri katika mwenendo wa ligi.

Kocha Arsene Wenger alisema kufungwa huko ni pigo kubwa kwa timu yake inayowania taji baada ya kukosa hata moja katika miaka minane iliyopita. Amekuwa akilaumiwa kwa uamuzi wake wa kuwapa wachezaji mapumziko ya siku mbili baada ya mechi dhidi ya Sunderland.

Katika mechi nyingine, Liverpool waliwafyatua Southampton 3-0 nyumbani kwao na kiupanda hadi nafasi ya pili ya msimamo wa ligi, wakiwa pointi sawa na Arsenal (59) lakini wanawaacha mbali kwa idadi ya mabao ya kufunga.

Mabao ya Liverpool yalifungwa na Luis Suarez, Raheem Sterling na penati ya Steven Gerald katika dakika ya 90.

Chelsea walizidi kupaa kwenye msimamo wa ligi wakiacha pengo la pointi nne baada ya kuwakanyaga Fulham 3-1, mabao ya Chelsea yakifungwa na Andre Schurrle na kuzidi kuwasababishia matatizo Fulham walio mkiani mwa ligi.

Katika mechi nyingine, Everton waliwafunga West Ham 1-0,  Newcastle wakawadungua Hull 4-1 wakati mechi  baina ya Sunderland na West Bromwich Albion imeahirishwa kwa sababu ya fainali ya Jumapili hii kati ya Sunderland na Manchester City katika Kombe la Ligi.

Comments