Chelsea watoa jasho kulinda heshima


Real Madrid wawakung’uta Schalke 6-1

Chelsea wamekwua timu pekee ya England katika raundi ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kuambulia pointi.

Wakicheza ugenini dhidi ya Galatasaray, Chelsea waliambulia sare ya 1-1 wakiwa ndio walitangulia kufunga kwa bao la Fernando Torres.

Wenyeji walisawazisha bao na kuweka mazingira sawa kwa mechi ijayo Stamford Bridge, baada ya Aurelien Chedjou kusawazisha dakika ya 62 akimpokonya mpira nahodha John Terry ambaye Mourinho amemrejesha tena kwenye kikosi cha kuanzia.

Vijana hao wa Jose Mourinho wamefuta kidogo aibu ya England, kwani timu nyingine tatu – Manchester United, Manchester City na Arsenal zilipigwa mabao 2-0 kila moja kwenye hatua hiyo.

Wakati Chelsea wakijitahidi kufurukuta, jambo ambalo halikuwa rahisi, Real Madrid nao katika hatua hiyo hiyo waliwakung’uta Schalke 6-1 na kujijengea mazingira ya kuingia robo fainali.

Chelsea ndio walitwaa kombe hilo 2012 na mechi hiyo imekuja siku chache baada ya Mourinho kunukuliwa akiwananga wachezaji wake, akidai hana mpachika mabao na kwamba huenda Samuel Eto’o ana miaka 35 na wala si 32.

Naye kocha wa Galatasaray, Roberto Mancini aliyewapatia ubingwa wa England Manchester City alinukuliwa kabla ya mchezo akisema kwamba hawangewafunga Chelsea katika mechi hiyo jijini Instanbul.

Arsenal, Manchester City na Manchester United waligawiwa dozi ya mabao mawili bila majibu na timu za Bayern Munich, Barcelona na Olympiakos katika mtiririko huo.

Mourinho alieleza masikitiko yake kwa nafasi walizopoteza kipindi cha kwanza akisema hakufurahishwa na matokeo lakini anayapokea tu wakati huu anapotafuta heshima ya kuwa kocha aliyefundisha timu tatu tofauti zikatwaa ubingwa wa UCL.

Comments