Manchester United maafa

*Wakong’otwa na Olympiakos 2-0

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England (EPL), Manchester United wameambulia kipigo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kutoka kwa vibonde, Olympiakos.

United ambao kwenye EPL wanafanya vibaya walisafiri hadi Ugiriki wakiwa na matumaini ya ushindi, hasa baada ya Wayne Rooney kusaini mkataba mpya.

Hata hivyo, Olympiakos waliwageuza asusa Mashetani Wekundu kwa kuwabandika bao kila kipindi na kumwacha kocha David Moyes akigugumia kwa maumivu.

Kuwatumia Rooney, Robin van Persie na wachezaji wengine wakongwe kama beki Rio Ferdinand, Patrice Evra na kipa David de Gea hakukuwasaidia maana walianza kupelekeshwa tangu mwanzo wa mchezo.

Katika mechi yote, Man U walifanikiwa kupiga shuti moja tu kwa shabaha langoni, wakati wapinzani wao walipata bao la kwanza kupitia kwa Alejandro Dominguez aliyezitikisa nyavu za United baada ya jitihada za mwenzake, Giannis Maniatis muda mfupi kabla ya mapumziko.

Mchezaji wa Arsenal anaycheza Olympiakos kwa mkopo, Joel Campbell aliwaumiza United hapo jijini Athens kwa shuti lake lililolenga vyema bao mapema kipindi cha pili.

RVP alipata nafasi ya wazi ya kufunga lakini akapaisha uu na kubaki akijilaumu.
Kichapo hicho kinafanya timu hiyo kuwa katika hatari ya kutolewa kwenye mashindano hayo makubwa, hivyo ama Moyes au baadhi ya wachezaji kuwa katika hatari ya kupoteza kibarua.

United, pasipo ubishi wowote, walicheza hovyo usiku huo wa Jumanne, wakishindwa kuanzia kukaba, kumiliki mpira, kushindwa kutwaa mipira ya juu na udhaifu mkubwa katika kushambulia.

Wachezaji wake walikuwa wakipokonywa mipira kirahisi na kuonekana kama vivuli vya wachezaji halisi aliowasajili Sir Alex Ferguson kabla ya kung’atuka.

Haijaeleweka bado tatizo la United ni lipi, kwa sababu wachezaji wote ndio wale wale waliocheza chini ya Fergie na kutwaa ubingwa msimu uliopita na kilichobadilika ni kocha tu.

Moyes alisema anabeba lawama kwa kupoteza mechi hiyo muhimu, na bila shaka atakuwa mwingi wa mawazo wanaposafiri kurudi Manchester ambapo bila shaka bodi itakuwa ikijiuliza kipi cha kufanya kuwaokoa, akikiri kwamba ni mchezo mbovu zaidi waliopata kucheza katikaUCL.

Comments