Barcelona wawafyatua Man City

Manchester City wameonja chungu ya kufungwa nyumbani, baada ya Barcelona kuwacharaza mabao mawili.

Licha ya kucheza vyema tangu mwanzo, Man City walijikuta wakianza kuwa nyuma kwa bao la penati, baada ya beki wao Martini Demichelis kumkwatua Lionel Messi katika eneo la penati.

Demichelis, beki anayependwa na kutegemewa sana na kocha Manuel Pellegrini alipewa kadi nyekundu, na Messi akafunga penati hiyo.

Palikuwa na dakika kadhaa za sintofahamu kwa City, ambapo Barca walitupiana pasi walivyotaka kwa muda mrefu.

Hata hivyo, City waligutuka tena na kurudia makali yake ya mwanzo wakaliandama lango la Barcelona kama nyuki bila mafanikio ya kupata bao.

Wakati mchezo ukielekea dakika ya 89, Barca walijaribu kwa mara nyingine shambulizi baada ya pasi za hapa na pale, na safari hii walifanikiwa kuwaliza City.

Alikuwa Dan Alvez aliyepita upande wa kulia na kipa Joe Hart alipotoka alifungishwa kwa tobo na kuandika usiku mchungu kwa City ambao walizoea kutesa timu nyingine hapo Etihad.

Inabidi wajipange upya sasa kwa safari ya Nou Camp ambako watahitaji kulipiza kisasi cha mabao hayo mawili kisha kutafuta la ushindi.

Katika mechi nyingine Jumanne hii, Paris Saint Germain (PSG) waliwasasambua Bayer Leverkusen nyumbani kwao Ujerumani kwa mabao 4-0 na bado watawasaubiri nyumbani kwao Ufaransa kumaliza ubishi mdogo uliobaki.

Jumatano hii jiji la London litawaka moto kwa pambano baina ya Arsenal na Bayern Munich katika dimba la Emirates.

Comments