Arsenal warudi kileleni

*Liverpool wabanwa na West Brom

Utamu wa Ligi Kuu ya England umefika pazuri kwa timu kuenguana kileleni, na Jumapili hii ilikuwa zamu ya Arsenal kuwaengua Manchester City.

Arsenal walifanikiwa kurudi kwenye nafasi waliyoishika kwa muda mrefu baada ya kuwafunga Crystal Palace 2-0 katika Uwanja wa Emirates.

Vijana wa Arsenal Wenger waliingia na mabadiliko kiasi kutokana na majeraha ya baadhi ya viungo wake na kadi nyekundu ya Mathieu Flamini.

Alex-Oxlade Chamberlain aliyetoka kwenye mapumziko ya maumivu karibuni alichezeshwa kiungo cha kati badala ya winga na kuwashambaza wachambuzi kabla ya mechi.

Hata hivyo, alikuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa England aliyefunga mabao yote mawili akishirikiana vyema na wenzake, akiwamo mshambuliaji wa kati, Mfaransa Olivier Giroud.

LIVERPOOL WAONESHA UCHOVU

Wakicheza na timu inayohatarika kushuka daraja ya West Bromwich Albion, Liverpool wanaowania ubingwa wa England au nne bora hawakucheza vyema.

Pamoja na kuwa na nyota wao, Luis Suarez, Daniel Sturridge waliokwishafunga zaidi ya mabao 40 kati yao na Raheem Sterling mwenye kasi na chenga za maudhi, walikumbana na ngome imara ya Baggies.

Hata hivyo, Sturridge alifanikiwa kumhadaa kipa Ben Foster baada ya kurushiwa mpira kwa mguu na pacha wake, Suarez ndani ya eneo la penati ambako wachezaji wa West Brom walishindwa kuuondoa kwa muda.

Bao hilo lilisawazishwa dakika chache kabla ya mpira kumalizika na Victor Anichebe aliyetokea benchi, baada ya beki wa Liverpool, Kolo Toure kutoa pasi mbovu kutoka pembeni kuelekea kati mwa goli, Anichebe akainasa na kumfunga Simon Mignolet kwa urahisi.

Usiku wa Jumatatu hii patachimbika katika dimba la Etihad pale Manchester City wanaofunga mabao kwa fujo watakapowakaribisha vijana wa Jose Mourinho, Chelsea.

Ni hapo itakapodhihirisha ipi ni soka ya karne ya 21 na ya 19, ambayo Mourinho aliwalaumu West Ham Jumatano iliyopita kwa jinsi walivyojenga ukuta imara.

Comments