Man United wamfuata Juan Mata


*Usajili wa Neymar wazua kesi Barcelona

Manchester United wamewasilisha dau la pauni milioni 35 kwa Chelsea ili kumsajili kiungo wao, Juan Mata.

Tangu Jose Mourinho arejee Stamford Bridge amekuwa hapendelei kumchezesha Mata (25) japokuwa msimu uliopita alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo hapo.

Pamoja na kwamba Man U wanakanusha kutoa ofa hiyo, inadaiwa mazungumzo yamefanywa na mawakala wa klabu hiyo ambapo wakikubaliana United wataweka nyaraka mezani ili wamchukue Mhispania huyo.

Jumatano hii Mata hakuwa kwenye kikosi cha kwanza katika mazoezi na Chelsea wamesisitiza kwamba Mata aliyetajwa kuwa mchezaji bora wa klabu hiyo kwa miaka miwili mfululizo hauzwi.

Mata alikuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania kilichoshiriki Kombe la Dunia 2010 na pia kwenye Michuano ya Ulaya 2012.
Inatarajiwa kwamba ofa hiyo ya awali itakataliwa na huenda Man U wanaohangaika kwenye nafasi mbaya katka ligi wakaongeza dau ili wajiondoe humo na kupanda kwenye nne bora kama si kutetea ubingwa wao.

USAJILI WA NEYMAR WAZUA KESI

Usajili wa nyota wa Brazil, Neymar uliofanywa na Barcelona umeleta kizaazaa na jaji anajiandaa kusikiliza kesi dhidi ya Rais wa Barcelona, Sandro Rosell.

Katika kesi hiyo ya aina yake, mwanachama wa Barca, Jordi Cases anadai kwamba kiasi halisi cha fedha kilichotolewa kilikuwa zaidi ya pauni milioni 48.6 na kwamba Rosell anafuja fedha za klabu.

Neymar (21) aliingia rasmi Nou Camp Juni mwaka jana akitoka Santos ya Brazil na Rosell anasema wanataka kupata ukweli juu ya kiasi kilichotumiwa na kwa ujumla kuelezwa akaunti ya matumizi ilivyo.

Rosell na wajumbe wengine wa bodi ya klabu hiyo wamekuwa wakidai kwamba vifungu vinavyoendekeza usiri kwenye katiba yao vinawazuia kujua ukweli wa mambo klabuni kwao.

Jaji Pablo Ruz ametaka apelekewe nyaraka kadhaa kuhusu uhamisho huo
Rosell aliyemrithi Rais Joan Laporta mwaka 2010 anasema kwamba yupo tayari kujibu maswali ya jaji kuhusu kesi hiyo na kwamba wanaheshimu mikataba yote waliyosaini.

Comments