Man City fainali Kombe la Ligi

Manchester City wametinga fainali ya Kombe la Ligi kwa mara ya kwanza katika miaka 38.
Vijana hao wa kocha Manuel Pellegrini wamefika kwa staili ya aina yake, baada ya kupata ushindi wa jumla ya mabao 9-0 dhidi ya West Ham katika mechi mbili za nusu fainali.
Hali hiyo inazidi kuwapa chati City wanaosifika msimu huu kwa idadi kubwa ya mabao ya kufunga kwa karibu kila mechi ambapo katika nusu fainali ya kwanza waliwakandika West Ham 6-0.
Usiku wa Jumanne ulikuwa mchungu kwa kocha Sam Allardyce ambaye amekumbana na vipigo mfululizo, pale Alvaro Negredo alipotikisa nyavu mara mbili na Sergio Aguero mara moja na kutosha kuwatupa vijana wake nje.
Hali ya hewa ilikuwa mbaya kwa West Ham waliocheza nyumbani Upton Park ambapo ilitarajiwa wangefungwa huku wakiwa pia katika nafasi za chini kabisa kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).
Kwa ushindi huo, City wanaingia Uwanja wa Wembley Machi 2 mwaka huu kwenye fainali ambapo watakabiliana na ama Manchester United au Sunderland kulingana na atakayeshinda kwenye nusu fainali nyingine Jumatano hii.
United walifungwa 2-1 katika mchezo wa kwanza.

Comments