Fifa yapendekeza kadi ya chungwa

Mgombea mtarajiwa wa urais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Jerome Champagne amependekeza kuanzishwa kwa kadi ya rangi ya chungwa.

Champagne (55) anayetaka kuchukua nafasi ya Rais Sepp Blatter anaona kwamba hiyo itakuwa njia mwafaka.

Kadi hiyo ya rangi ya chungwa itatolewa kwa mchezaji aliyefanya kosa ambalo si kubwa kiasi cha kumtoa nje kabisa.kwa kadi hiyo, mchezaji ataelekezwa kwenda kukaa nje kwa muda wa dakika kadhaa kisha atarudi uwanjani.

Hiyo hufanyika kwenye mchezo wa rugby na hockey, ambapo mwamuzi hunyoosha mikono yote miwili na kumwelekeza mchezaji kwenda kwenye benchi husika kama adhabu na timu hairuhusiwi kumbadili mchezaji huyo hadi atakaporejea uwanjani.

Kadhalika, Champagne anataka timu ziadhibiwe pale wachezaji wao wanapowahoji waamuzi kama ilivyo kwenye mchezo wa rugby ambapo manahodha tu ndio hutakiwa kuzungumza nao.

Kadhalika, Mfaransa huyu anatarajia kwamba soka itatumia teknolojia zaidi katika kufikia uamuzi muhimu.
Uchaguzi mkuu wa Fifa umepangwa kufanyika Zurich, Uswisi Juni mwaka kesho.

Hata hivyo, Champagne anasema hana uhakika kama atagombea iwapo Blatter (77) ataamua kuwania tena kiti hicho kwa msimu wa tano na anasema Blatter ni mtu mwenye ushawishi mkubwa na alishamweleza juu ya nia yake ya kugombea.

Champagne anaungwa mkono na gwiji wa zamani wa soka wa Brazil, Pele na alitangaza uamuzi huo Jumatatu hii jijini London. Mgombea mwingine anayetarajiwa ni Mfaransa Michel Platini anayeongoza Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa).

Comments