Yaya Toure mwanasoka bora

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limemtangaza kiungo wa Manchester City na Ivory Coast, Yaya Toure kuwa mwanasoka bora wa mwaka.
Toure amepata tuzo hiyo kwa mwaka jana, ikiwa ni mara ya tatu mfululizo na pia alichaguliwa Desemba kuwa mwnaasoka wa mwaka wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Alikuwa akiwania tuzo hiyo na raia mwenzake wa Ivory Coast, mshambuliaji Didier Drogba anayechezea Galatasaray na kiungo Mnigeria wa Chelsea, ohn Mikel Obi.

Toure (30) amefuata nyayo za Abedi Pele na Samuel Eto’o waliopata kutwaa tuzo hiyo miaka mitatu kama yeye alivyotwaa kuanzia 2011 hadi 2013.

Eto’o alikuwa mwanasoka bora wa 2010, mwaka mmoja kabla alikuwa Didier Drogba, wakati 2008 alikuwa Emmanuel Adebayor. Mwaka 2007 alitwaa Frederic Kanoute na 2006 ilikuwa zamu ya Drogba.

Pele alishinda tuzo hiyo kati ya 1991 na 1993 wakati Eto’o ilikuwa kuanzia 2003 hadi 2005.

Toure amekuwa kwenye kiwango cha hali ya juu kwa klabu na nchi yake na alipewa tuzo yake jijini Lagos, Nigeria japokuwa hajapata kombe lolote kwa klabu wala nchi yake mwaka jana.

Huyu ndiye Mwafrika pekee aliyeorodhshwa miongoni mwa wanasoka 23 wa kuwania mwanasoka bora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Mpinzani wake wa karibu, Mikel (26) aliwasaidia Nigeria kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana na pia alikuwa kwenye kikosi cha Chelsea kilichotwaa kombe la Ligi ya Europa.

Nwanko Kanu, nahodha msaidizi wa zamani wa Arsenal ndiye Mnigeria wa mwisho kupata tuzo kama hii, nayo ilikuwa mwaka 1999. Drogba alikuwa mshindi wa pili mwaka jana.

Comments