Kombe la Dunia Qatar Novemba – Desemba

Hatimaye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limetangaza kwamba Kombe la Dunia 2022 halitafanyika majira ya joto nchini Qatar.
Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke amesema kwamba haitawezekana michuano hiyo mikubwa zaidi kufanyika wakati huo kutokana na kiwango kikubwa cha joto.

Rais wa Fifa, Sepp Blatter alipata kudokeza awali kwamba ingekuwa vigumu kuchezwa wakati huo ambapo joto hupanda hadi zaidi ya nyuzijoto 50.

Wadau wengi waliilaumu Fifa kwa kupanga michuano hiyo wakati huo Mashariki ya Kati na pamekuwapo na nadharia kwamba mlungula ulitembea katika kuipa nchi hiyo uenyeji.

Wadau wengine wamekuwa wakipinga kubadilishwa muda wa mashindano kwa maelezo kwamba kutavuruga ratiba za mambo mengine huku Qatar wenyewe wakidai kwamba wangeweka mashine maalumu za kupoza joto uwanjani.

Sasa inatarajiwa kwamba mashindano hayo yatafanyika kati ya Novemba 15 na Desemba 15, 2022, muda ambao rais na katibu mkuu wa Fifa wamedokeza.

“Tarehe za Kombe la Dunia (Qatar) hazitakuwa Juni-Julai 2022, ukweli ni kwamba nadhani mashindano yatafayika kati ya Novemba 15 na Desemba 15, maana ndicho kipindi hali ya hewa ni nzuri zaidi kwenye nyuzijoto 25 hivi,” alisema Valcke kupitia Radio France.

Comments