Arsenal safi, Man United hoi


*Moyes amlalamikia refa Howard Webb
*Man City, Chelsea, Liverpool washinda

Mabao mawili yaliyofungwa dakika za mwisho yamewawezesha Arsenal kubaki katika kilele cha msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Mabao hayo yalitiwa kimiani na mshambuliaji wa kati anayetaka kuondoka Emirates, Nicklas Bendtner na Theo Walcott ambaye tangu atoke kwenye kujiuguza amekuwa moto wa kuotea mbali.
Ushindi huo unawafanya Arsenal kufikisha pointi 45, mbili juu zaidi ya Manchester City ambao pia katika mechi ya mwaka mpya walipata ushindi wa 3-2 dhidi ya Swansea.
Mabingwa watetezi, Manchester United wameendelea kupoteza mechi baada ya kukubali kichapo cha 2-1 katika dimba la Old Trafford.
Mabao ya wageni yalitiwa kimiani na Emmanuel Adebayor aliyeanza kucheza tangu kufukuzwa kazi kwa kocha Andre Villas-Boas na Eriksen wakati la United lilifungwa na Danny Welcbeck.
Kwa kupoteza mechi hiyo Mashetani Wekundu wanashika anfasi ya saba huku Tottenham wakiwa ya sita.
Kocha wa Man U, David Moyes amemlaumu mwamuzi Howard Webb kwa madai ya kuinyima timu yake penati kwa madai kwamba Ashley Young aliangushwa na kipa Hugo Lloris wakati akienda kufunga.
Chelsea nao walipata ushindi dhidi ya Southampton kwa jumla ya mabao 3-0 na kuwaweka vijana hao wa Jose Mourinho katika nafasi ya tatu.
Liverpool wapo nafasi ya nne baada ya ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Hull, ikiwa ndio wametoka kupata vipigo mfululizo mara mbili.
Katika mechi nyingine, Crystal Palace walikwenda sare ya 1-1 na Cardiff, Fulham wakawafunga West Ham 2-1, Stoke wakaenda sare ya 1-1 na Everton, Sunderland wakazidi kuachwa mkiani kwa kufungwa na Aston Villa 1-0 huku West Bromwich Albion wakiwapiga Newcastle 1-0.
Timu zinazoshika nafasi za mkiani ni Crystal Palace wenye poinyi 17, West Ham pointi 15 na Sunderland pointi 14.

Comments