Chelsea watibuliwa na Sunderland


*Watupwa nje ya Kombe la Ligi
*Man City waingia nusu fainali

Mawazo ya ‘kawaida’ ya Chelsea kuingia nusu fainali ya Kombe la Ligi yaligeuka ndoto ya mchana baada ya kutibuliwa na Sunderland.
Wakiongoza kwa bao 1-0 hadi kuelekea mwisho wa mchezo, Chelsea walijikuta wakiadabishwa na mchezaji wao wa zamani, Fabio Borini aliyeingia kipindi cha pili na kutikisa nyavu zao.

Bao la Chelsea lilifungwa mara tu baada ya kuanza kipindi cha pili na Frank Lampard, ambapo kwa mara ya kwanza kwenye michuano hii teknolojia ya goli ilitumika.

Lampard anatambulika kwa bao lake kwa England dhidi ya Ujerumani kukataliwa kutokana na macho ya mwanadamu kushindwa kuona vyema.

Lakini usiku wa Jumanne hii mwamuzi hakuwa na tabu, bali kifaa alichovaa mkononi kilimwonesha kwamba ni bao, licha ya kipa Tito Mannone kuuvuta mpira haraka kutoka nyuma ya mstari.

Wakati timu zikielekea kukamilisha kipindi cha pili huku kocha wa Chelsea, Jose Mourinho akijidai kwa kutembea tembea eneo lake la kujidai, Borini aliwaadhiri dakika ya 88

Walipoingia katika muda wa zaida, walitoshana nguvu huku kila upande ukikosa mabao na alikuwa mchezaji wa Korea, Ki Sung-Yueng aliyewatesa mabeki, akageuka na kuweka mpira kimiani dakika ya 118.

MANCHESTER CITY NUSU FAINALI

Manchester City wameingia nusu fainali ya Kombe la Ligi msimu huu.

Man City wanaofundishwa na Manuel Pellegrini walivuka baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya vijana wa Leicester City wanaocheza kwenye Championship.

Man City wanaojulikana zaidi siku hizi kwa mtindo wao wa kuachia mvua ya mabao wakiwa nyumbani, lakini jioni ya Jumanne hii walikuwa ugenini.

Kwa hiyo matatu kutoka kwa Aleksandar Kolarov na Edin Dzeko aliyefunga mawili, yaliwatosha wakati wenyeji walipata bao la kufutia machozi kutoka kwa Lloyd Dyer.

Jumatano hii katika robo fainali nyingine, Stoke watakuwa wenyeji wa Manchester United wakati Tottenham Hotspur waliomfukuza kocha wao, Andre Villas-Boas watakabiliana na West Ham kwenye dimba lile lile ambalo Liverpool waliwanyoa 5-0 Jumapili hii.

Comments