Man City waisambaratisha Arsenal

Manchester City wameendeleza dozi kubwa kubwa nyumbani kwao baada ya kuwafunga vinara wa ligi Arsenal 6-3.

United walitoa ujumbe mkali kwa washindani wao kwa mabao ya Sergio Aguero, Alvaro Negredo, mawili ya Fernandincho, David Silva na penati ya Yaya Toure dakika ya 90.

Arsenal walijaribu kujibu mashambulizi kwa kukata nusu ya mabao hayo kupitia kwa Theo Walcott aliyerejea baada ya majeraha na kufunga mawili na beki Per Metersacker aliyefunga dakika za majeruhi.

Arsenal wanakuwa timu ya kwanza pia kufunga mabao mengi kiasi hicho Etihad, kwani Man City wamekuwa wakisambaratisha timu hapo kwa mabao mengi bila majibu ya kuridhisha.

Hata hivyo, kufungwa huko kumeapunguza kasi sana Arsenal, hasa baada ya kwenda sare na Everton mechi iliyopita ya ligi, ambapo sasa pengo la pointi tano walilokuwa wameweka limebaki mbili tu.

Chelsea ndio wapo nyuma yao baada ya jana kuwafunga kwa tabu Crystal Palace 2-1 na kufikisha pointi 33 huku Man City wakiwa nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 32.

Cardiff waliwafunga West Bromwich Albion 1-0, ikiwa ni mechi ya nne mfululizo kwa West Brom kupoteza na hivyo kuamua kumfukuza kazi kocha wake mkuu, Steve Clarke.

Everton waliwasambaratisha Fulham kwa 4-1 na kufikisha pointi 31 katika nafasi ya nne, Newcastle wakaenda sare ya 1-1 na Southampton, West Ham na Sunderland wakaambulia suluhu kama ilivyokuwa kwa Hull na Stoke.

Comments