Van Persie nje mwezi mzima

Msimu unaelekea kuzidi kwenda kombo kwa Robin van Persie na klabu yake ya Manchester United, baada ya kutangazwa atakuwa nje ya dimba kwa mwezi mzima.

RVP alishakuwa nje kwa mwezi mzima kutokana na majeraha ya kidole kabla ya kuanza mechi dhidi ya Newcastle ambapo United walitandikwa bao 1-0.

Kocha David Moyes amesema mchezaji huyo aliumia nyama za paja wakati akipiga kona dhidi ya Shakhtar Donetsk Jumanne iliyopita.
RVP alikuwa mfungaji bora akiwa nahodha wa Arsenal kabla ya kuhamia United msimu uliopita ambapo pia aliibuka mfungaji bora wa ligi kuu akiwa na mabao 26.

Hata hivyo, msimu huu Van Persie (30) ameanza kwa kusuasua na sasa ameumia tena, hali aliyopata kuwa nayo akiwa Arsenal.
Katika kipindi ambacho hatakuwa uwanjani, Man U watacheza mechi nane na Moyes anasema ni pigo kwake kwa sababu ushirika wake na Wayne Rooney ulikuwa mzuri sana.

Alisajiliwa United kwa pauni milioni 24 lakini baada ya msimu mmoja tu kocha aliyemvutia, Sir Alex Ferguson akastaafu, jambo linaloelezwa pia kumchanganya kwani hakutarajia.

Hadi sasa amefunga mabao saba tu katika mechi 11 za ligi alizocheza. Mbali na RVP, Man United pia wana majeruhi mwingine, Marouane Fellaini anayeumwa mgongo lakini anatarajiwa kurejea si muda mrefu kutoka sasa.

Nemanja Vidic, Patrice Evra na Chris Smalling hawakuchezeshwa mechi dhidi ya Shakhtar lakini Moyes anasema kwamba anacho kikosi cha wachezaji wengi wenye uwezo watakaoweza kuziba pengo lolote.

United wanashika nafasi ya tisa na ni msimu mbaya zaidi kwao kwa muda mrefu uliopita. Jumapili hii wanasafiri hadi Birmingham kwa ajili ya kukabiliana na Aston Villa kwenye mechi ya ligi baada ya kupoteza mechi mbili nyumbani na kuwa pointi 13 nyuma ya vinara wa ligi Arsenal.

Comments