Gareth Bale aanza hat-trick

Mchezaji ghali zaidi duniani, Gareth Bale amefanikiwa kufunga mabao matatu katika mechi moja (hat-trick) tangu ajiunge na Real Madrid.
Amefanya hivyo huku nyota wa timu hiyo aliyezoeleka kwa hat-trick, Cristiano Ronaldo akiwa mgonjwa na kushindwa kucheza.

Ilikuwa ni katika mechi dhidi ya Real Valladolid, ambapo Real Madrid walishinda kwa mabao 4-0, bao jingine likifungwa na Karim Benzema asiyetakiwa na mashabiki Santiago Bernabeu.

Kujeruhiwa kwa Ronaldo kulimfanya Bale kutupiwa macho yote Jumamosi hii, ambapo alifunga bao la kwanza, akamtengea Benzema kufunga la pili kabla ya mwenyewe kupiga mawili ya mwisho na kuondoka na mpira.

Hat-trick hiyo imekuja muda mfupi baada ya kampuni ya Audi kukabidhi magari ya kifahari kwa wachezaji na kocha wao, Carlo Ancelotti, ambapo wachezaji waligawanywa kuendana na kile kinachoonekana umaarufu wao.

Ronaldo alipewa gari ya ghali zaidi, akifuatiwa na Xabi Alonso, Sergio Ramos kisha kundi la wengi alimokuwa Bale, hivyo kuonesha wazi kwamba licha ya kununuliwa kwa fedha nyingi, bado Ronaldo anathaminiwa zaidi.

Hata Bale, baada ya mechi hiyo alisema kwamba bado Ronaldo ndiye bora, hata katika kufunga mabao mengi kwa mchezo mmoja kiwastani.
Ushindi huo wa Real umewasogeza pointi tatu nyuma ya vinara Barcelona wanaocheza na Athletic Bilbao Jumapili hii. Barca wana pointi sawa na Atletico Madrid.

Bale alinunuliwa kwa pauni milioni 85 kutoka Tottenham Hotspur msimu wa usajili wa majira ya joto mwaka huu. Ronaldo amefunga mabao 32 msimu huu katika mechi 22 tu.

Comments