Steven Gerrard kuwa beki?

 
*Kocha asema atacheza miaka mingi

 
Liverpool haifikirii kwamba nahodha wake, Steven Gerrard anakaribia kustaafu katika umri wake wa miaka 33.

Badala yake, Kocha Brendan Rodgers anafikiria kumpa majukumu mapya kama beki badala ya nafasi yake ya sasa ya kiungo ili kuwapaisha zaidi Liverpool.

Gerrard amekuwa kichocheo kikubwa kwenye kiungo, hasa msimu huu na kidogo uliopiya, maana katika misimu mingine ya nyuma kidogo mambo yalikuwa mazito kwa Liverpool.

Gerrard amekuwa akikiri kwamba umri unakwenda, lakini bado anapenda kuendelea kuitumikia klabu ambayo amekuwa kama injini yake kwa muda mrefu.

Hayo yanakuja wakati Ryan Giggs wa Manchester United aliyetinga umri wa miaka 40 wikiendi hii akisema bado anafikiria kuendelea na soka na kwamba anajua mwenyewe atakapotundika daluga.

Ni kawaida kwamba wachezaji wenye umri mkubwa wamekuwa mabeki, japokuwa wapo viungo na washambuliaji, lakini makipa ndio zaidi ya wote kwa umri mkubwa na umahiri hata katika timu za taifa.

Kocha Rodgers anafikiri kwamba Gerrard akihama kutoka kiungo kurudi nyuma kwenye beki, hasa ya kati, anaweza kuweka rekodi nzuri kwa kucheza muda mrefu lakini pia kwa kuwasaidia Liverpool kupata matokeo mazuri.

“Nikimwangalia Steven naona kwamba angeweza kuwa kama beki wa kati baadaye, nadhani anaweza kucheza kama beki wa kati upande wa kulia,” anasema bosi wake huyo.

Gerrard amebaki Liverpool katika Jua na mvua, raha na shida pasipo kuhama licha ya kutakiwa na Manchester United na klabu nyingine.

Gerrard alisaini mkataba mpya wa miaka miwili unusu katika msimu wa majira ya joto mwaka huu, ambapo anatarajiwa kuendelea kucheza Liverpool hadi baada ya kufikisha umri wa miaka 35.

Huyu ndiye pia nahodha wa timu ya taifa ya England ambaye alianza rasmi kukipiga kama mchezaji wa kulipwa 1998 na maisha yote ya soka ya kulipwa amekuwa Anfield.

Rodgers (40) anasema kwamba anaamini Gerrard anaweza kuwasaidia zaidi kama atajenga msingi wa soka ya Liverpool kutoka eneo hilo la nyuma kwa sababu anajua kuwapanga wenzake, ana usahihi wa pasi na pia husonga mbele kwa mashambulizi.
 

Comments