Ivory Coast, Nigeria Kombe la Dunia

 
Ivory Coast na Nigeria zimekata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Nigeria ambao ni mabingwa wa Afrika walikuwa wa kwanza kufuzu baada ya kuwafunga Ethiopia 2-0 katika mechi iliyopigwa Calabar Jumamosi hii.

Victor Moses na Victor Obinna ndio walikuwa wauaji katika ushindi ambao Nigeria wamewatoa Ethiopia kwa jumla ya mabao 4-1.

Moses alifunga kwa penati baada ya Aynalem Hailu kudaiwa kushika mpira, japokuwa katika mazingira tata.

Nigeria wameingia fainali hizo kwa mara ya tano, baada ya kufuzu katika miaka ya 1994, 1998, 2002 na 2010 na watakwenda Brazil wakitaka kuvuka hatua za mtoano kama walivyofanya 1998. Eagles sasa watakuwa chini ya Kocha Stephen Keshi aliyekuwa nahodha Nigeria walipofuzu kwa mara ya kwanza.

Ivory Coast walikata tiketi yao baada ya kwenda sare ya 1-1 na Senegal kwenye mechi iliyopigwa Casablanca,Morocco, kutokana na Senegal kufungiwa kwa sababu ya fujo.

Matokeo hayo yanawafanya Ivory Coast kuwa na uwiano mzuri wa mabao 4-2 kutokana na ushindi walioupata kwenye mechi ya awali.

Ivory Coast walikuwa nyuma kwa bao moja, na alikuwa Salomon Kalou aliyefunga bao muhimu dakika za mwisho na kuwahakikishia safari ya Brazil.

Senegal walipata bao kwa njia ya penati kupitia kwa Moussa Sow lakini kusawazishwa kwake kunawafanya Tembo hao kujipanga kwa fainali hizo maana 2006 na 2010 walikuwa kwenye makundi magumu.

Cameroon Jumapili hii wanawakaribisha Tunisia wakati Jumanne Burkina Faso watavaana na Algeria huku Misri wakitakiwa kupata mabao matano dhidi ya Ghana ili kufufua matumaini ya kwenda Brazil.
 

Comments