Penati ya Chelsea yawasha moto


*West Brom wataka waamuzi wapitie video

Penati waliyopewa Chelsea dakika ya mwisho ya majeruhi na kupata sare dhidi ya West Bromwich Albion imewasha moto.

West Brom sasa wanaitaka Bodi ya Ligi Kuu kutoa mkanda wa video wa tukio hilo na ipitiwe kwenye kikao cha wadau.

Wanapendekeza pia kwamba katika utata kuhusu penati, waamuzi wawe na fursa ya kupitia video kabla ya kutoa au kukataa penati, na hoja hiyo inatarajiwa kujadiliwa baadaye.

Chelsea walikuwa nyuma 1-2 dhidi ya Baggies ndipo mwamuzi akatoa penati baada ya Ramires kugongana na Steven Reid na mwamuzi akatoa penati tata.

Jeremy Peace, Mwenyekiti wa West Brom, timu iliyowafunga Manchester United na kutoa sare na Arsenal ameandika barua rasmi kwa bodi hiyo.

Licha ya mechi hiyo, Peace anasema wanataka mapitio ya uamuzi kwenye mechi nyingine wanazoamini walionewa na kama si hivyo wangekuwa mbele kwa pointi saba na katika nafasi ya tano badala ya 10 wanayoshikilia.

Kocha Steve Clarke wa West Brom alikasirishwa sana na kitendo cha kutolewa penati hiyo wakati Chelsea wakiwa wanazama nyumbani kwao Stamford Bridge, lakini Jose Mourinho anadai ilikuwa penati stahili kwao.

Michezo mingine ambayo West Brom wanadhani kwamba hawakutendewa haki ni dhidi ya Southampton, Arsenal na Stoke.

Mwenyekiti amemwomba Mike Riley, Mkuu wa Taasisi ya Soka ya Kulipwa na Waamuzi wa Mechi kutoa ufafanuzi wa maamuzi yote hayo mabovu.

Comments