Al Ahly bigwa Afrika

Al Ahly wa Misri wametwaa ubingwa wa Afrika baada ya kuwashinda Orlando Pirates kutoka Afrika Kusini.

Ahly walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano ya fainali iliyochezwa katika dimba la Arab Contractors jijini Cairo Jumapili hii.

Ahly wamefanikiwa kutetea taji hilo licha ya machafuko ya kisiasa nchini humo ambayo yamefikia hatua ya kuathiri hata soka.

Ushindi wa Jumapili hii unamanisha kwamba Ahly wamekuwa kifua mbele kwa mabao 3-1 kwani katika mechi ya awali iliyofanyika Afrika Kusini walishinda 1-0.

Mahasimu wao, Zamalek, waliweka kando tofauti za utani wa jadi na kuwaambia washabiki wao wawashangilie Ahly, jambo ambalo ni muhali kutokea Tanzania pale Simba au Yanga wanapocheza na timu za nje.

Alikuwa mchezaji mkongwe, Mohamed Aboutrika aliyepachika bao la kwanza katka dakika ya 54 nje kidogo tu ya lile boksi la yadi sita.

Wakati Pirates wakifikiria jinsi watakavyopata mabao mengi kufidia, Ahmed Abdul Zaher alipachika bao la pili na msumari wa mwisho kwenye jeneza la wageni katika dakika ya 78 na kumwacha hoi kipa Senzo Meyiwa.

Furaha ya mabingwa hao wa Misri ilipungua baada ya mchezaji wao, Sherif Abdel Fadil kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Daine Klate.

Pirates walipata kuwa mabingwa wa Afrika 1995. Hii ilikuwa mechi ya kwanza kubwa nchini Misri baada ya mechi nyingi kuhamishiwa kwingine, kutokana na machafuko yaliyosababisha watu 74 kuuawa uwanjani, wengi wao wakiwa washabiki wa Ahly.

Comments