Penati tata yawaokoa Chelsea


*Liverpool wapaa, kocha Fulham matatani
*Southampton safi, leo Man U na Arsenal
 

Mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu ya England umeanza kwa namna tofauti, ambapo penati ya utata iliwaokoa Chelsea kuzama kwa West Bromwich Albion.

Chelsea walianza kupata bao kupitia kwa Samuel Eto’o mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kosa kubwa la beki kufagia hatari, lakini lilisawazishwa na bao kuongezwa kipindi cha pili kupitia kwa Shane Long na Stephane Sessegnon.

West Brom wakiwa wageni Stamford Bridge walipata bao ambalo hata washabiki wa Chelsea walijua ni la ushindi lakini dakika ya mwisho ya mchezo mwamuzi Andre Marriner alitoa penati yenye utata iliyofungwa na Eden Hazard.

West Brom walilalamikia penati hiyo, maana ilionekana kwamba Steven Reid aligongana na Ramires ndani ya eneo la hatari naye kwenda chini kirahisi na mwamuzi kuamua iwe penati iliyowatibua nyongo wageni.

Sare hiyo imemfanya Jose Mourinho kuendeleza rekodi yake msimu huu wa ligi pasipo kufungwa nyumbani na timu yake inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi nyuma ya Arsenal, Liverpool na Southampton.

Katika mechi nyingine jijini Liverpool, wenyeji waliwafyatua Fulham mabao 4-0 na kuongeza shinikizo kwa kocha wa vijana hao wa London kwamba huenda akafutwa kazi muda ujao.

Alikuwa tena Luis Suarez aliyesababisha cheche kwa upande wa Liverpool kwa kufunga katika dakika ya 36 na 54 baada ya Fernando Amorebieta kujifunga mwenyewe na jingine likifungwa na mwana Liverpool, Martin Skrtel.

Matokeo hayo yamewaacha pabaya vijana wa Jol, kwani wanashika nafasi ya 17, ikiwa ni ya nne kutoka mkiani, huku Stoke walio chini yao wakiwa bado wana mchezo mkononi, hivyo kuwapo uwezekano wa kuwashusha kwenye eneo la hatari.

Katika matokeo mengine, Aston Villa walipata ahueni kwa kuwafunga Cardiff 2-0; Crystal Palace wakaonesha udhabiti kwa kwenda suluhu na timu ngumu ya Everton, Southampton wakiwakwaruza Hull mabao 4-1 na Norwich wakiuona mwanga kwa kuwakung’uta West Ham 3-1.

Kivumbi Jumapili hii ni kati ya Tottenham na Newcastle mchana, Sunderland na Manchester City, Manchester United na Arsenal na Swansea dhidi ya Stoke.

Bado Crystal Palace wanaburuza mkia kwa pointi zao nne sawa na za walio juu yao Sunderland wakifuatiwa na Stoke wenye pointi tisa.
 

Comments