Man U ushindi kidogo, muhimu!

 
Manchester United wamepata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Real Sociedad.
Wakicheza nyumbani katika Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Jumatano, Man U walifanya kazi ya ziada kuepuka sare au kichapo, na hata bao lao walisaidiwa na mchezaji wa Sociedad, Inigo Martinez aliyejifunga katika dakika ya pili tu ya mchezo.

Walau ushindi huo ni faraja kwa kocha David Moyes ambaye ana wakati mgumu katika Ligi Kuu ya England, na Jumamosi iliyopita aliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Southampton katika dimba la Old Trafford.

Mechi hiyo imekuja muda mfupi baada ya kocha aliyeng’atuka Manchester, Alex Ferguson kuzindua kitabu cha wasifu wake na masuala ya soka.

Sociedad waligangamala mbele ya washabiki wao 6,000 waliosafiri kutoka kwao wanakocheza Ligi Kuu ya Hispania – La Liga. United walishika roho zao pale mkwaju wa Antoine Griezmann ulipogonga mwamba, nusura asawazishe bao.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo ya mabingwa,  RSC Anderlecht waliangukia pua mbele ya Paris Saint Germain walipochabangwa 5-0, CSKA Moscow wakalala 2-1 nyumbani walipowakaribisha Manchester City na Bayern Leverkusen wakawakandamiza Shaktar Donetsk  4-0.

Galatasaray ya Roberto Mancini walipata ushindi wa 3-1 dhidi ya FC Copenhagen, Real Madrid wakawafunga Juventus 2-1, Benfica wakaenda sare ya 1-1 na Olympiakos wakati Bayern Munich wakiwagaragaza Viktoria Plzen 5-0.

Comments