Kagera yaipania Yanga Kaitaba…

Uwanja wa Kaitaba ulikuwa mgumu kwa Yanga katika misimu miwili iliyopita kwani ilifungwa dhidi ya Kagera Sugar. Msimu uliopita ‘Wanajangwani’ walilala 1-0 dhidi ya ‘Walimamiwa wa Kagera’, mchezo ambao ulikuwa wa kwanza kwa kocha Mholanzi Ernie Brandts baada ya kurithi mikoba ya kocha Mbelgiji Tom Saintfiet aliyetimuliwa baada ya kukiongoza kikosi cha Yanga katika mechi mbili tu za ligi kuu walizotoka suluhu dhidi ya Prisons kabla ya kupokea kichapo cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa.

Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Hamis Madachi, alisema kikosi chao ambacho kimeshinda mechi tatu tu kati ya saba msimu huu tayari kimeanza mazoezi maalum kwa ajili ya kuikabili Yanga Jumamosi.

Alisema wanatambua kwamba Yanga ni timu ngumu na imeimarika baada ya kuanza vibaya msimu kwa sare tatu mfululizo, ndiyo maana wamebadili hata ratiba ya timu yao kwa kufanya mazoezi mara mbili kila siku badala ya mara moja ilivyokuwa awali.

“Timu ilirejea jana (juzi) kutoka Dar es Salaam na imeingia kambini kukusanya nguvu kabla ya kuikabili Yanga. Yanga hawajapata ushindi hapa (Kagera) kwa misimu miwili mfululizo. Tumejipanga kuhakikisha hawatoki na pointi Jumamosi,” alisema Madachi.

Kagera Sugar, ambayo msimu uliopita ilikuwa chini ya kocha Abdallah Kibadeni ‘King’ (sasa kocha wa Simba) imekusanya pointi 11 katika michezo saba msimu huu wakati Yanga ina pointi 12, tatu nyuma ya vinara Simba.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuwa kikosi chao kilichoanza mazoezi kwa ajili ya kuiwinda Kagera jana, kitaanza safari kuelekea Kanda ya Ziwa leo

Comments