Uzembe Afrika waisononesha Fifa

 
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limesikitishwa na hali ya mataifa kadhaa ya Afrika kutokuwa makini kiasi cha kuchezesha wachezaji wasiotakiwa.

Fifa imesema inasononeshwa na jinsi timu zinavyokiuka kanuni za wachezaji wasiotakiwa kucheza, tena kwenye mechi za kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014.

Mkurugenzi wa Mashindano wa Fifa, Mustapha Fahmy anasema inasikitisha kuona kwamba mechi nane zimebadilishwa matokeo kutokana na moja ya timu kwenye kila mechi kuchezesha mchezaji aliyezuiwa kwa sababu ya kadi nyekundu.

Katika mechi zote, timu pinzani na ile iliyochezesha mchezaji asiyetakiwa ilipewa ushindi wa mabao 3-0 na pointi tatu na kuathiri kwa kiasi kikubwa misimamo kwenye makundi.

Anasema hajui tatizo liko wapi kwani kanuni zipo wazi na kwamba siku zote Fifa wamekuwa wakitoa ushirikiano ili mashindano yote yaende vizuri.

Cape Verde wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na tatizo hilo, ambapo licha ya kufanya vyema sana kwa mara ya kwanza kwenye kufuzu huko na kuwashinda Tunisia 2-0 jijini Tunis, waliadhibiwa na kupokonywa mabao na pointi zote na kutupwa nje ya mashindano kwa kuchezesha mchezaji aliyekuwa anatumikia adhabu.

Guinea ya Ikweta nayo ilipoteza pointi tatu kwa sababu hiyo hiyo walipocheza na Cape Verde kabla.
 

Comments