Pigo la kwanza kwa Mourinho


*Arsenal waongoza ligi, Man U washinda

 

Kocha Mkuu wa Chelsea, Jose Mourinho ‘The Happy One’ ameonja pigo la kwanza kwenye Ligi Kuu ya England.

Chelsea wamelala kwa bao 1-0 kutoka kwa Everton wanaofundishwa na Roberto Martinez, ukiwa pia ni ushindi wake wa kwanza msimu huu, akiwa ametoka klabu ya Wigan iliyoshuka daraja.

Bao la kichwa la Steven Naismith siku yake ya kuzaliwa katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza lilitosha kumliza Mourinho licha ya kuchezesha nyota wake, akiwamo Samuel Eto’o.

Everton walikuwa wametoa sare mechi zao tatu za mwanzo baada ya kuachana na David Moyes ambaye amerithi mikoba ya Alex Ferguson Manchester United.

Mwamuzi Howard Webb alimudu vyema mchezo huo, na mechi ilipomalizika, Goodison Park ililipuka kwa nderemo na vifijo kwa wachezaji wao.

Katika mechi nyingine, Arsenal waliosafiri hadi Sunderland walifanikiwa kuwafunga vijana wa Paolo Di Canio kwa mabao 3-1 na kukamata uongozi wa ligi.

Mshambuliaji Mfaransa Olivier Giroud aliendelea kung’ara kwa kufunga bao moja, huku kiungo Mwingereza, Aaron Ramsey akifunga mawili na mchezaji aliyesajiliwa kutoka Real Madrid, Mesut Ozil akiwa msaada mkubwa.

Manchester United nao walifanikiwa kuchomoza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Crystal Palace katika dimba la Old Trafford, Aston Villa wakilala nyumbani kwa mabao 2-1 kutoka kwa Newcastle.

Sare kadhaa zilishuhudiwa, ambapo Fulham na West Bromwich Albion walitoka bao 1-1 kama ilivyokuwa kwa Hull na Cardiff huku Stoke City wakiwakamata Manchester City kwa suluhu.
Tottenham Hotspur walifaidi kwa mabao 2-0 dhidi ya Norwich na kuendelea kuwang’ang’ania majirani zao wa kaskazini mwa London.

Kwa matokeo hayo, Arsenal wanaongoza ligi kwa pointi tisa wakifuatiwa na Spurs na Liverpool weye idadi hiyo hiyo ya pointi.

Man City, Man United, Stoke na Newcastle wana pointi saba kila mmoja wakati Everton wakiwa na pointi sita na Cardiff pointi tano.

West Ham United wanashika nafasi ya 11 wakiwa na pointi nne kama zilivyo klabu za Southampton, Fulham, Norwich na Hull.

Aston Villa na Crystal Palace wana pointi tatu wakiguatiwa na Swansea kwa idadi hiyo hiyo ya pointi wakati West Brom wana pointi mbili na Sunderland moja tu kutokana na mechi nne.

Comments