Mathieu Flamini arejea Arsenal

*Ligi ya Mabingwa Ulaya makundi yatajwa

 

WAKATI kiungo wa zamani wa Arsenal, Mathieu Flamini amerejea Emirates, makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) yametajwa.

Flamini (29) anaingia Arsenal kutoka AC Milan ya Italia akiwa mchezaji wa pili kusajiliwa msimu huu baada ya Yaya Sanogo (20) aliyetoka Auxerre ya Ufaransa.

Flamini alicheza Arsenal kwa miaka minne tangu mwaka 2004 akitoka Marseille ya Ufaransa ambayo ni raia wake na akiwa na Arsenal alicheza mechi 102 na kupata heshima kubwa
Mbali na kucheza kama kiungo mkabaji, ni kiraka anayeweza kucheza kama beki wa kulia na kushoto, kwenye nafasi za akina Bacary Sagna na Kieran Gibbs.

ETO’O AJIUNGA CHELSEA

Mchezaji wa kimataifa wa Cameroon aliyekuwa akichezea klabu ya Urusi ya Anzhi Makhachkala, Samuel Eto’o amejiunga na Chelsea.

Eto’o mwenye umri wa miaka 32 anajiunga na Chelsea baada ya Manchester United kukataa kumwachia mpachika mabao wake, Wayne Rooney, licha ya Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho kutoa ofa mbili na kutaka kuongeza kumpata.

Eto’o anaweza kusaidia safu ya ushambuliaji ya Chelsea yenye watu kama Fernando Torres, Romelo Lukaku na Demba Ba, ambao hata mmoja wao hakuanzishwa kwenye mechi kubwa dhidi ya Manchester United mwanzoni mwa wiki hii.

MAKUNDI LIGI YA MABINGWA HADHARANI

20130829-210217.jpg

Hatimaye Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) limetoa ratiba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), ambapo katika kundi A kuna klabu za Manchester United, Shakhtar Donetsk, Bayer Leverkusen na Real Sociedad.

Kundi B linajumuisha timu za Real Madrid, Juventus, Galatasaray na FC Copenhagen wakati C kuna Benfica, Paris St-Germain, Olympiakos na Anderlecht.

Mabingwa watetezi, Bayern Munich wapo katika kundi D wakiwa na klabu za CSKA Moscow, Manchester City na Viktoria Plzen huku kundi E likiwa na Chelsea, Schalke, FC Basel na Steaua Bucharest.

Washika Bunduki wa London – Arsenal wamepangwa na Marseille, Borussia Dortmund na Napoli kwenye kundi F wakati lile la G kuna Porto, Atletico Madrid, Zenit St Petersburg na Austria Vienna.

Kundi la mwisho la H lina wababe Barcelona watakaooneshana kazi na AC Milan, Ajax na Celtic ya Uskochi, ambayo mwaka jana pia walikuwa kundi moja na Barca. Mechi za mzunguko wa kwanza kwenye makundi hayo zinatarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 17 na 18 mwaka huu.

 

Comments