Arsenal, Liverpool watakata


*Stoke, Hull wang’ara, wengine sare

 

Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya England umekuwa wa kicheko kwa Arsenal walioanza vibaya awali, ambapo Jumamosi hii wamewakung’uta Fulham 3-1.
Wakicheza ugenini Craven Cottage, Arsenal walipata mabao kupitia kwa washambuliaji wake Olivier Giroud wakati Lukas Podolski alitupia moja kila kipindi.

Arsenal wanaofundishwa na Arsene Wenger na waliosajili mchezaji mmoja tu mpya, Yaya Sanogo bure waliwakabili vilivyo Fulham wa Martin Jol wenye wachezaji wanane wapya.

Alikuwa mmoja wa hao wanane, Darren Bent aliyekuwa Aston Villa msimu uliopita aliyefanikiwa kufuta machozi kwa bao moja, baada ya kazi kubwa ya Dimitar Berbatov.

20130824-205730.jpg

Katika mechi nyingine, Liverpool walipata ushindi wa pili mfululizo kwa kuwafunga Aston Villa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Daniel Sturridge, ikiwa ni mara ya kwanza katika miaka mitano wameshinda mechi zao mbili za mwanzo wa ligi.
Kipa wa Liverpool, Simon Mignolet aliyesajiliwa na kocha Brendan Rodgers kutoka Sunderland majira haya ya kiangazi, alifanya kazi ya ziada kuzuia hatari zilizoelekezwa langoni mwake na Villa, hasa zile za mshambuliaji wa Kibelgiji, Christian Benteke.

Mechi nyingine iliyokuwa na mshindi ilishuhudia Stoke City wanaofundishwa na Mark Hughes waliofanikiwa kuchomoa bao walilofungwa mapema na Crystal Palace na kuongeza la ushindi.

Mchezaji wa zamani wa Arsenal, Marouane Chamakh aliwafungia Crystal Palace lakini bao hilo likarudishwa na Charlie Adam kabla ya Shawcross kupachika bao la ushindi. Palace wamepoteza mechi zote mbili hadi sasa.
Katika mechi nyingine, Everton walitoshana nguvu na West Bromwich Albion kwa kwenda suluhu wakati Hull waliwafunga Norwich bao 1-0.

Newcastle walioanza vibaya kwa kufungwa mabao manne na Manchester City walimudu kutoka suluhu walipowakaribisha Wrst Ham huku Southampton wakitoka sare ya bao 1-1 na Sunderland.

Cardiff watawakaribisha Manchester City Jumapili hii wakati Tottenham Hotspur ni wenyeji wa Swansea huku Jumatatu kikiwa kivumbi baina ya Manchester United na Chelsea.

Comments