Arsenal watuliza mzuka Uturuki


*Wawatandika Fenerbahce 3-0
*Chelsea waipiga Vila kwa tabu

Baada ya kuteswa kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England, Arsenal wameipoteza klabu ngumu ya Fenerbahce nyumbani kwao Uturuki.
Katika mechi ya kutafuta kufuzu kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, vijana wa Arsene Wenger waliingia kwa kujiamini na kudhamiria kuchukua ushindi, na waliupata wa aina yake wa mabao 3-0.
Wakicheza kwenye uwanja ambao awali vyombo vya habari vya Uingereza viliufananisha na jehanamu, Arsenal waliutawala mchezo kwa jumla ya asilimia 59 dhidi ya 41 jijini Istanbul.
Arsenal wamejiwekea mazingira mazuri ya kutinga hatua ya makundi, kwani watahitaji sare ya aina yoyote au ushindi kwenye mechi ya marudiano Emirates siku sita baada ya mechi hii.
Baada ya kufungwa mabao 3-1 na Aston Villa hapo Emirates Jumamosi iliyopita, Arsenal wamekabiliwa na kelele za washabiki wanaotaka kuona wakisajili nyota.
Kumalizika kwa kipindi cha kwanza ugenini hapo timu zikiwa suluhu, kulisababisha wageni kuanza kuonekana kupata shinikizo la kufunga.
Alikuwa beki wa kushoto, Kieran Gibbs aliyedaka majalo ya The Walcott na kuitundika kambani dakika ya 51, kabla ya Aaron Ramsey kuachia shuti umbali wa yadi 20 na kumteleza kipa Volkan Demirel.
Mshambuliaji tegemeo siku hizi wa Arsenal, Olivier Giroud alionekana kurejea kujiamini tena, kwani baada ya kufunga bao Jumamosi dhidi ya Villa, jijini Istanbul alifunga penati baada ya Michal Kadlec kumchezea rafu Walcott.

CHELSEA WASHINDA VILLA KWA MBINDE

20130821-222657.jpg

Katika mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili wa EPL Chelsea walipata ushindi uliolalamikiwa na Aston Villa, kwani walinyimwa penati ambayo wangeweza kusawazisha mambo.
Wakicheza nyumbani Stamford Bridge chini ya Jose Mouriho ambaye hajapata kufungwa hapo, Chelsea walionekana kuwa na bahati kuliko wageni, walipomaliza mechi kwa ushindi wa mabao 2-1.
Mkwaju wa Eden Hazard ulisukumizwa kimiani kwa bahati mbaya na mchezaji wa Villa, Antonio Luna dakika ya saba kabla ya Christian Benteke kuwainua vitini wana Villa kwa kusawazisha dakika ya 45.
Alikuwa mchezaji mwenye bahati ya kufunga mabao muhimu ya ushindi, Branislav Ivanovic aliyepiga mpira mzito wa kichwa katika dakika ya 73 na kuandika bao lililotokea kuwa la ushindi kwa Chelsea.
Hata hivyo, ilielekea kwamba Villa wanaofundishwa na Paul Lambert walistahili ushindi, pale John Terry alipozuia kwa mkono mpira wa kichwa uliopigwa na Gabriel Agbonlahor lakini mwamuzi Kevin Friend kupeta tu.
Mourinho na Lambert walionekana kupandishiana hasira kwenye eneo lao la ufundi, Lambert akilalamika. Katika mechi zake nyumbani, Mourinho alishinda 48 na kutoa sare 14 na alizopoteza zilikuwa ugenini.
Desemba mwaka jana, Villa walikung’utwa mabao 8-0 na Chelsea, ambapo ni wachezaji sita tu waliocheza siku hiyo walipangwa Jumatano hii.

 

Enhanced by Zemanta

Comments