Manchester United Ngao ya Jamii

Mabingwa watetezi wa England, Manchester United wamempa kocha mpya, David Moyes zawadi kwa kutwaa Ngao ya Jamii.

Katika mechi iliyokipigwa katika Uwanja wa Wembley dhidi ya klabu inayoshushwa daraja msimu uliopita ya Wigan, Mdachi Robin van Persie alipachika mabao mawili na kumwondolea shaka kocha huyo Mskochi.

Moyes amekuwa katika majadiliano juu ya hatima ya Wayne Rooney, mchezaji aliyemzindua akiwa Everton kisha akaja kumkuta Man U, lakini ameshaomba zaidi ya mara moja kuondoka.

Ushindi huo umekuwa liwazo Old Trafford, kwa vile katika mechi ya kwanza ya Moyes hapo, walifungwa mabao 3-1 na Sevilla ya Hispania majuzi.

Moyes ameweka wazi kwamba chaguo lake la kwanza kwa mshambuliaji wa kati ni RVP na kwamba Rooney anaweza kusota benchi, lakini Mwingereza huyo anadhani muda aliokaa hapo unatosha.

Iliwachukua Man U dakika sita tu kupata bao la kwanza na baada ya hapo Wigan wanaofundishwa na Owen Coyle waligangamala. Hata hivyo dakika ya 59 ilikuwa tena chungu kwao, kwani Mdachi huyo aliyehamia United kutoka Arsenal msimu uliopita, alipachika bao la pili.

Enhanced by Zemanta

Comments