Bale: Nataka kwenda Real Madrid


*Spurs huenda wakapewa Di Maria na Coentrao

Hatimaye shinikizo limeanza White Hart Lane, bada ya nyota wao tegemeo, Gareth Bale kuweka wazi nia yake ya kuihama klabu ya Tottenham Hotspur.
Bale (26) mzaliwa wa Wales anayecheza kama winga, kiungo na mpachika mabao kiongozi wa Spurs, ameweka wazi nia yake ya kuhamia Real Madrid wanaomtaka.
Madrid wanaonolewa na kocha mpya Carlo Ancelotti, ametaka wawakilishi wake wazungumzena Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy, ambaye kama kocha Andre Villas-Boas, alipata kusema hawatamuuza mchezaji huyo wa kimatafa wa Wales.
Real Madrid wapo tayari kutoa ofa itakayovunja rekodi ya dunia, pauni milioni 86.3, ambalo Bale anaamini bado lipo mezani kwa wakubwa wake, na haoni kwa nini suala hilo lisijadiliwe.
Levy kwa muda mrefu hataki kusikia nyota wake huyo anaondoka, na alizungumza naye kwa muda mfupi Hong Kong. Levy alikwenda Marekani anakomiliki mali, lakini amesharejea London kwa ajili ya kusimamia mwenyewe suala hilo zito.
Bale na wachezaji wenzake wamerejea kutoka Asia walikokwenda kwa ajili ya ziara ya kujifua kabla ya msimu mpya unaoanza mwezi ujao, ambapo Villas-Boas amewapa mapumziko ya siku mbili.
Bale hakucheza kwenye mechi hizo za Mashariki ya Mbali, kwani ana maumivu madogo ya mguu, Villas-Boas akisema angeanza mazoezi wiki hii, ambapo awali alisema atahakikisha mchezaji wake huyo atabaki White Hart Lane.
Spurs wamedhamiria kuchelewesha dili hili, kama walivyofanya kwa Luka Modric aliyeenda Madrid na Dimitar Berbatov ambaye hatimaye alikwenda Manchester United na sasa yupo Fulham.
Bale alihamia Spurs kutoka Southampton mwaka 2007, lakini kiwango chake cha sasa kimekuja msimu uliopita, baada ya Villas-Boas kujiunga Spurs, na mwenyewe Bale anakiri Mreno huyo ndiye amemkunja inavyotakiwa.
Spurs wenyewe wanasema mazungumzo kati yao na Bale kuongeza mkataba wake na kuboresha mafao yake ili apate pauni 150,000 kwa wiki, lakini wanaelekea kugonga mwamba, kwani Bale anataka kuchezea klabu kubwa zaidi na pia kushiriki Klabu Bingwa Ulaya.
Licha ya mpango wa fedha, Real Madrid wapo tayari kumchukua mchezaji huyo na kuwapa Spurs winga wa Argentina, Angel Di Maria na beki Fabio Coentrao. Dili za aina hiyo ni ngumu, maana hushirikisha watu wengi, na itategemea ukubali wa wachezaji na mawakala wao.

Comments