Ratiba EPL hadharani


*Man United kuanzia Swansea, Arsenal na Aston Villa
*Man City na Newcastle, Mourinho kuwakaribisha Hull

Ratiba ya kipute cha Ligi Kuu England (EPL) imetoka, ambapo mabingwa Manchester United wanaanza kwa kibarua nchini Wales, watakakokwaana na Swansea.
Huo utakuwa mtihani wa kwanza katika mashindano makubwa, kwa kocha mkuu mpya, David Moyes, aliyechukua nafasi ya Sir Alex Ferguson aliyeng’atuka. Wachambuzi wa mambo wanasema Moyes atakuwa na wakati mgumu kumudu mazingira mapya ya kazi yake, maana ni tofauti mno na alivyokuwa Everton, klabu ya kati, yenye matumizi madogo.
Kocha mwingine mpya kwenye klabu za EPL ni Jose Mourinho ambaye anaanza kampeni yake nyumbani, hiyo hiyo Agosti 17 Chelsea watakapomenyana na timu mpya iliyopandishwa daraja ya Hull City.
Mechi ya kwanza kwa mhandisi Manuel Pellegrini aliyeajiriwa Manchester City itakuwa dhidi ya Newcastle kwenye dimba la Etihad. Cardiff ya Wales iliyopanda daraja msimu huu watasafii hadi London kupepetana na West Ham United, wakati wageni wengine, Crystal Palace watacheza na Tottenham Hotspur.
Ratiba hiyo inaonesha kwamba, Arsenal ya Arsene Wenger watawakaribisha Aston Villa; Liverpool watakuwa nyumbani kucheza na Stoke; wakati Everton watakaribishwa Norwich.
Paolo Di Canio atakuwa nyumbani Sunderland kukipiga na Fulham wakati West Bromwich Albion watawakaribisha Southampton.
Wakati huo huo, fainali ya Kombe la FA imerejeshwa kwenye eneo lake la zamani, nalo ni mwishoni mwa msimu wa ligi ya EPL, ambapo mechi ya fainali kwa mwakani imepangwa kupigwa Mei 17, wiki moja baada ya msimu wa ligi kumalizika.Msimu wa 2010 ndio ulikuwa wa mwisho kwa ratiba hiyo kufuatwa.

Comments