Chelsea wahitaji pointi moja


*Benteke awagharimu Villa

Chelsea wamekaribia kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kupata pointi tatu muhimu kwa jasho na damu nyumbani kwa Aston Villa, walipowafunga mabao 2-1.
Mabao ya The Blues yalifungwa na kiungo Frank Lampard, hivyo kuweka rekodi kwa kuwa mfungaji bora zaidi wa muda wote Chelsea, kwani amefikisha mabao 203, moja zaidi ya aliyekuwa akishika rekodi hiyo, Bobby Tambling.
Licha ya kuwafungia bao la ndani ya dakika 15 za kwanza, kosa la Christian Benteke kunyanyua guu lake dhidi ya nahodha wa Chelsea, John Terry na kupewa kadi nyekundu, limewagharimu Aston Villa.
Hilo lilikuwa kosa la pili kwa Benteke, hivyo kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu katika robo ya kwanza ya kipindi cha pili, na kuacha timu zote zikiwa na wachezaji 10 kila moja, kwani Ramires wa Chelsea naye alitolewa, baada ya kufanya rafu zinazokadiriwa kufika tano katika nusu ya kwanza ya mchezo.
Matokeo hayo yanawafanya Chelsea wahitaji pointi moja kujihakikishia nafasi ligi hiyo kubwa ya Ulaya, kwani wamefikisha pointi 72 wakiwa wamebakisha pointi moja dhidi ya Everton. Arsenal wana pointi 67 na wakishinda mechi zao mbili dhidi ya Wigan na Newcastle United watafikisha pointi 73.
Tottenham Hotspurs wenye pointi 66 wakishinda mechi zao dhidi ya Sunderland na Stoke watafikisha pointi 72. Kwa msingi huo, majaliwa ya Spurs hayapo mikononi mwao, bali watategemea Chelsea au Arsenal kupoteza pointi.
Villa wanashika nafasi ya 13 wakiwa na pointi 40 na nyuma yao wapo Southampton wenye pointi 39; Sunderland, Norwich na Newcastle wenye pointi 38 na Wigan walio hali mbaya na pointi zao 35. Reading na QPR wameshashuka daraja, hivyo anatafutwa msindikizaji mmoja wafunge safari kuondoka EPL.

Comments