Sunderland wapigana kiume


*Kifo chawachungulia Wigan, Newcastle, Norwich

Kocha Mtaliano mwenye mbwembwe, Paolo Di Canio ametoka dimbani kwa furaha, baada ya vijana wake – Sunderland kuibuka na sare dhidi ya Stoke City, licha ya kucheza karibu theluthi mbili ya mchezo wakiwa 10.
Sunderland waliruhusu bao la mapema la dakika ya tisa kutoka kwa Jonathan Walters na wakati wakijaribu kurudisha bao hilo mbele ya maelfu ya washabiki wao, walipata pigo la pili kubwa kwa Craig Gardner kutolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kutokana na rafu mbaya dhidi ya Charlie Adam.
Hata hivyo, Di Canio anayejulikana kwa tambo zake akiwa dimbani tangu zamani, alionekana mwingi wa mawazo, na kila baada ya muda akitoa maelekezo kwa wachezaji wake, hivyo kwamba alifikia kukanyaga dimba badala ya kukaa eneo walilotengewa makocha.
Maelekezo yake yaliekelea kuzaa matunda, kwani Sunderland ambao mechi iliyopita walipoteza mchezaji – Stephane Sessegnol – kwa kadi nyekundu pia, walitulia, kujiamini na kufanikiwa kutawala mchezo, hasa kipindi cha pili na kumpa wakati mgumu kocha Tony Pulis wa Stoke.
Baada ya kosa kosa kadhaa, John O’Shea aliwasawazishia Black Cats katika dakika ya 63 kutoka umbali wa yadi tano tu baada ya kunasa mpira wa Sebastian Larsson na nusura Danny Rose awapatie bao la ushindi dakika chache baadaye.
Licha ya kuambulia pointi moja tu, imekuwa muhimu kwa Sunderland, kwani imewapandisha hadi nafasi ya 15, wakiwa juu ya Norwich na Newcastle, na pia ikiwaacha juu ya Wigan walio nafasi ya kushuka daraja kwa ponti tatu.
Baada ya Reading na Queen Park Rangers (QPR) kushuka daraja, Wigan wanatakiwa kufanya kazi ya ziada, kwani wana pointi 35 na mechi tatu mkononi, huku Norwich, Newcastle na Sunderland wakiwa nazo 38 na mechi mbili mbili mkononi.
Ikiwa Wigan watafanya vyema kwenye mechi zake zilizobaki, hata Southampton wenye pointi 39 na Aston Villa wenye 40 wanaweza kuvutwa kuondoshwa kwenye Ligi Kuu ya England.

Comments