Aston Villa wawaachia Wigan zigo

Baada ya Reading na Queen Park Rangers (QPR) kushuka daraja, Aston Villa wameelekea kuwaachia matatizo Wigan kwa kujipatia pointi tatu muhimu.
Wigan ndiyo timu ya tatu inayokaribia kushuka daraja, ikiwa na pointi 32, tofauti na 25 walizo nazo Reading na QPR na sasa wameachwa kwa pointi tano na Villa.
Vijana hao wa Paul Lambert walipata pointi hizo tatu katika ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya Sunderland jijini Birmingham katika mchezo pekee wa Jumatatu.
Mabao ya Villa yalifungwa na Christian Benteke matatu, Gabriel Abonlahor, Ron Vlaar na Andreas Weiman, wakati lile la Sunderland lilifungwa na Danny Rose.
Lambert aliyehangaika kwa muda mrefu kuwaondoa Villa matatizoni, amepata ahueni kwa ushindi huo, kwani mchezo uliopita walicharazwa 3-0 na Manchester United walipotangazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya England.
Villa wamewaachia nafasi ya 17 Newcastle United, wanaolingana nao pointi, tofauti ikiwa kwenye uwiano wa mabao, ambao nao ni bao moja tu. Sunderland wana afadhali kuliko timu hizo mbili, kwani licha ya kuwa na pointi hizo hizo, wana uwiano mzuri zaidi wa mabao kwa alama 10.
Kocha wa Sunderland, Paolo Di Canio aliyefurahia ushindi dhidi ya Newcastle na Everton tangu ajiunge na klabu hiyo, alikuwa amefananisha pambano la Jumatatu hii na fainali ya Ligi ya Mabingwa, lakini pia alitabiri kwamba mambo yalikuwa yameanza kwenda vibaya.
Timu nyingine iliyo maeneo ya chini ni Norwich, wanaowazidi Sunderland kwa pointi moja na Southampton walio juu pointi moja zaidi.

20130429-225949.jpg

Enhanced by Zemanta

Comments